NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Barrick, kupitia Mgodi wake wa North Mara, imeanza kutekeleza kwa vitendo ahadi iliyotolewa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Mark Bristow la kurekebisha kipande cha barabara korofi katika eneo la vijiji vya Nyamongo na Kewanja wilayani Tarime mkoani Mara, iliyokuwa imeharibika sana na kuleta usumbufu mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo wanaotumia barabara hiyo.
Kipande hicho kinachokarabatiwa na Barrick, kina umbali wa kilometa 3.6 kuanzia katika kijji cha Kewanja kwenye kitongoji cha Kwinogo, kuanzia makutano ya barabara ya kwenda Serengeti, hadi kwenye makutano ya barabara ya kwenda Tarime.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wakiongelea hatua hiyo jana baada ya kushuhudia mkandarasi kampuni ya ujenzi ya Stanley, ameanza kazi ya kuchonga na kumwaga vifusi, walisema kuwa barabara hiyo iliharibika na kuwasababishia usumbufu mkubwa na hasara na walishukuru uongozi wa Barrick kwa ukarabati wa barabara hiyo.
Naye Samwel Wambura, akiongea kwa niaba ya madereva wa vyombo vya moto wanaotumia barabara hiyo alisema kuwa kwa muda mrefu imewasababishia hasara kubwa ya kuharibika kwa vyombo vyao na alishukuru Barrick kwa kuona umuhimu wa kuifanyia ukarabati ili iweze kupitika vizuri.
Kwa upande wake, Meneja Mahusiano ya Kijamii wa Mgodi wa North Mara, Gilbert Mworia, alisema barabara hiyo inakarabatiwa kutokana na ombi la viongozi wa eneo hilo pia kutokana na ubovu wake uliosababisha utumiaji wa barabara za mgodini kuwa mkubwa hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya Wananchi kutokana na barabara nyingi za Mgodini kutumiwa na mitambo mikubwa ya shughuli za uchimbaji.