NA GODFREY NNKO
AFISA Mtendaji Mkuu (CEO) wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez ametuma salamu za pole kwa Wanasimba baada ya kupoteza mechi ya Ngao ya Jamii kwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga SC.
Ni kupitia mtanange wa nguvu uliopigwa Agosti 13, 2022 katika dimba la Bejamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
“Poleni sana Wanasimba; kuteleza sio kuanguka. A luta continua,”ameandia Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC,Bi.Gonzalez kupitia mitandao yake ya kijamii.
Pole hizo zinakuja, baada ya Yanga SC jana katika dakika 45 za kwanza za mtanange huo kuambulia patupu kutokana na bao lililotumbukizwa nyavuni na winga Msenegal, Pape Ousmane Sakho ndani ya dakika ya 16.
Sakho alifunga bao zuri dakika ya 16 baada ya kuutokea vizuri mpira wa adhabu uliopigwa na Clatous Chotta Chama na kumshinda kipa wa Yanga SC, Djigui Diarra.
Kipindi cha pili Yanga SC ilizinduka na mshambuliaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Fiston Kalala Mayele akafunga bao la kwanza dakika ya 50 akimalizia pasi ya kiungo Stephanie Aziz Ki na la pili dakika ya 80 baada ya kuwachambua mabeki watatu wa Simba kufuatia pasi ya, Khalid Aucho.
Nderemo
"Azizi, Azizi,Azizi...Azizi, Azizi, Azizi....Azizi, Azizi, Azizi," ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam waliskika mashabiki wa Yanga mara kwa mara wakiimba jina la staa huyo aliyesajiliwa kutoka ASEC Mimomas ya Ivory Coast, ambapo alimaliza ligi kuu nchini humo akitwaa tuzo ya mchezaji bora huku akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji ghali zaidi.
Aidha, tangu aanze kutumika kama namba 10 katika kipindi cha pili alionekana kuwa na madhra zaidi kwa Simba SC tofauti na awali ambapo alikuwa akitokea pembeni.
Aidha, Yanga SC ambao ni mabingwa wa Ngao ya Jamii Yanga kwa mwaka uliopita baada ya kutetea ubingwa huo kwa kuwafunga watani wao wa jadi Simba SC, huenda huu ukawa ni mwanzo mzuri mwingine kwao.