Dar yatangaza tena msako mifuko ya plastiki

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla ameelekeza operesheni ya kukamata mifuko ya plastiki iliyokatazwa kuanza rasmi Jumatatu ya Agosti 29, 2022 kwenye masoko yote ya mkoa huo.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi na viongozi wa masoko yote ya mkoa huo, machinga na Maafisa Masoko ambapo pia ameelekeza msako wa kukamata Viwanda Bubu vinavyozalisha mifuko hiyo kuanza mara moja.

Aidha, RC Makalla ameelekeza kila wilaya kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama kuendesha operesheni hiyo ambapo pia amewataka Maafisa Masoko kwa kila soko kutoa taarifa ya mwenendo wa zoezi hilo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika kila siku.

Tayari RC Makalla amepata baraka zote za operesheni hiyo kutoka kwa Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango ambaye ameelekeza kila mkoa kufanya operesheni ya kutokomeza na kuzuia uingiaji wa Mifuko hiyo.
Pamoja na hayo RC Makalla ameelekeza Mamlaka za Udhibiti ikiwemo Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutoa tamko la maelekezo ya usimamizi kwa kila mkoa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa.

Juni Mosi, 2019 Serikali ilitangaza marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki na kufanikiwa, lakini hivi karibuni mifuko hiyo imeanza kurudi kwa kasi jambo lililopelekea Serikali kutangaza operesheni ya kutokomeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news