'Dhamira ya Rais Samia kwa vyombo vya habari ni njema, tunaamini tutafanikiwa'

NA MWANDISHI WETU

“Awali Serikali haikuonesha dhamira ya kushughulikua maoni ya wadau wa habari nchini, lakini katika utawala huu wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan dhamira imeoneshwa tangu mwanzo, tunaamini tutafanikiwa;

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Neville Meena ameyasema hayo wakati akizungumza na Dodoma FM ya jijini Dodoma kuelezea kuhusiana na michakato mbalimbali inayoendelea ili maboresho ya sheria za habari nchini yaweze kutekelezeka kwa wakati.

Bw.Meena ambaye pia ni Katibu mstaafu wa TEF amesema,Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 iliacha mambo ya msingi katika kukuza tasnia ya habari na badala yake ikawa ni sheria ambazo ni ngumu kutekelezwa.

Amesema, kutokana na kuwepo kwa mazingira magumu ya habari na wanahabari nchini, tasnia ya habari iliyumba kwa kiwango kikubwa.

“Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipingwa na wadau wa habari siku moja baada ya kupitishwa ili kutumika. Si kwamba, hakukuwa na vitu muhimu kwa wanahabari, wadau waliona imebeba mitego na madhara mengi kwa wanahabari na vyombo vya habari,’’amesema Bw.Meena

Amesema kuwa, kuna lawama zinaelekezwa kwa vyombo vya habari kukosa weledi, moja ya changamoto inayovikabili ni kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati.

Meena ansaema, vyombo vya habari vinashindwa kulipa mishahara kwa kuwa, watangazaji wengi hasa Serikali kwenye halmashauri,wanatoa matangazo lakini hawataki kulipa hivyo kuchangia kushuka kwa weledi kwenye vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vinalalamikiwa kukosa weledi, lakini tukumbuke kwamba wanaotoa matangazo na kushindwa kulipa, wanachangia kutengeneza tatizo.

“Wanaoongoza kutolipa ni wakurugenzi wa halmashauri, hili linachangia kuyumbisha vyombo vya habari na ndio maana tumependekeza baada ya miezi sita mtangazaji kushindwa kulipa, licha ya kukumbushwa basi afikishwe mahakamani,’’amesema.

Pia amesema, ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kutaka wadau wa habari wakutane na kuchakata mapendekezo ya sheria za habari imetimia.

“Suala la mapendekezo yote ya wadau wa habari kupita, hilo ni suala lingine. Cha msingi ni kwamba, miongoni mwa ahadi za Rais (Samia Suluhu Hassan), ikiwemo wizara kukutana na wadau wa habari na kupitia vifungu, imetekelezwa.

“Sisi kama wadau wa habari tunaamini tunakwenda kufanikiwa kwa kuwa, hata Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) ana hisia chanya katika mchakato huo,’’amesema.

Amesema, miongoni mwa mapendekezo ya wadau wa habari katika mabadiliko ya sheria za habari nchini, ni kuwa uamuzi wa mahakama uwe unaheshimiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news