HII HAPA ORODHA YA MASWALI YA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2022

NA MWANDISHI MAALUM

KWA mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), maswali yote ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 yanatakiwa kujibiwa na Mkuu wa Kaya husika, isipokuwa MASWALI YA HALI YA UZAZI kuanzia swali Namba 67 hadi 71 ambayo yanatakiwa yajibiwe na mwanamke mwenyewe mwenye umri wa miaka 10 au zaidi.

MAANA YA MKUU WA KAYA: Kwa madhumuni ya Sensa, Mkuu wa Kaya ni mtu yeyote mzima ambaye watu wote walio katika kaya husika wanamtambua kama Mkuu wa Kaya hiyo.

MAANA YA KAYA: Kwa madhumuni ya Sensa, kaya ni jumla ya watu ambao kwa kawaida huishi na kula pamoja (yaani hushirikiana katika kupata mahitaji yao ya kila siku).

Inawezekana kaya kuwa ni mume, mke, watoto na ndugu wengine, wageni na watumishi katika kaya nao wahesabike kama watu wa kaya hiyo iwapo walilala kwenye kaya husika usiku wa kuamkia siku ya Sensa.

Ikiwa mtu anaishi na kula peke yake, basi, ahesabiwe kama kaya ya mtu mmoja hata kama anakaa katika nyumba ya watu wengi.

A. SWALI LA 1 HADI 68 NI KWA WATU WOTE WALIOLALA KWENYE KAYA USIKU
WA KUAMKIA SIKU YA SENSA

1. Tafadhali nitajie majina ya watu wote waliolala katika kaya hii usiku wa kuamkia siku ya Sensa, yaani usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne ya tarehe 23 Agosti, 2022, ukianzia na jina la Mkuu wa Kaya.

Majibu ya swali hili yataiwezesha Serikali kupata idadi ya watu wote nchini na wastani wa idadi ya watu katika kaya.

2. Je, una uhusiano gani na Mkuu wa Kaya?

Majibu ya swali hili yataiwezesha Serikali na wadau wengine kupata takwimu zitakazoonesha hali halisi ya kiwango cha utegemezi ndani ya kaya, kaya zinazoongozwa na wanawake, na kaya zinazoongozwa na watoto kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo.

3. Je, wewe ni mwanamme au mwanamke?

Majibu ya swali hili yatawezesha kujua idadi ya wanaume na wanawake katika kila Kaya, kila Kitongoji, Kijiji/Mtaa, Kata/Shehia, Wilaya, Mkoa na pia Taifa kwa ajili ya mipango ya maendeleo.

4. Je, una umri wa miaka mingapi?

Umri ni taarifa muhimu sana katika takwimu za watu kwenye Taifa lolote lile duniani. Kwa kujua umri, Serikali itaweza kupanga Mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, maji, maendeleo ya jamii na mengine mengi kwa kuzingiatia mahitaji kulingana na umri wa watu wa maeneo husika.

5. Ni ipi hali ya ndoa yako kwa hivi sasa? Hujaoa, umeoa, mnaishi pamoja, umeachana,umetengana, umefiwa na mke/mume?

Swali hili litaulizwa kwa watu wote wenye umri wa miaka 10 au zaidi. Majibu ya swali hili yataiwezesha Serikali kujua idadi ya watu katika jamii wenye ndoa pamoja na halizi za ndoa hizo na wale wasio na ndoa ambapo kwa kujumuishwa na takwimu zinazotokana na maswali mengine, Serikali na wadau wengine itaweza kupanga mipango ya maendeleo ya kimkakati ya watu wake.

6. Tafadhali nitajie namba yako ya simu ya mkononi

Swali hili linalenga kupata namba ya simu ya kila mwanakaya, mwenye umri wa miaka 15 au zaidi. Majibu ya swali hili yatasaidia kutengeneza kanzidata ya watu ambayo inaweza kutumiwa kufanya tafiti kwa njia ya simu. Tafadhali weka kumbukumbu ya namba ya simu kwa wale wote wenye umri wa miaka 15 au zaidi.

Kama huna Namba ya Simu unayomiliki andika namba ya mtu yeyote unayoitumia kwa mawasiliano ili kusaidia kukupata endapo utachaguliwa kushiriki kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

7. Je, una ualbino?

8. Je, una matatizo ya kuona hata ukiwa umevaa miwani?

9. Je, una matatizo ya kusikia hata kama unatumia shimesikio?

10. Je, una matatizo ya kutembea au kupanda ngazi?

11. Je, una matatizo ya kukumbuka au kufanya kitu kwa umakini?

12. Je, una matatizo ya kujihudumia kama vile kuoga au kuvaa nguo?

13. Je, una matatizo ya Kuwasiliana kwa kutumia lugha ya kawaida?;kwa mfano kuelewa au
kueleweka?

14. Je, una aina nyingine ya ulemavu?

Maswali ya 7 hadi 14 yanalenga kupata taarifa za hali ya ulemavu katika jamii. Majibu ya maswali haya yataiwezesha Serikali kujua idadi ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali nchini na hivyo kuweza kuweka mipango endelevu kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu kulingana na mahitaji yao.

15. Je, ni nini chanzo cha ulemavu ulionao?

Majibu ya maswali haya yataisaidia Serikali kupanga mipango ya kukabiliana na sababu zinazosababisha ulemavu

16. Je, una kifaa saidizi kwa tatizo/ulemavu ulionao?

Majibu ya Maswali haya yataisaidia Serikali kupata idadi ya watu wenye ulemavu wenye vifaa saidizi na wasiokuwa na vifaa saidizi ili kutambua ukubwa wa mahitaji uliopo

17. Je, wewe ni raia wa nchi gani? IWAPO NI RAIA WA NCHI MBILI: Je, ni raia wa nchi zipi?

Majibu ya swali hili yataiwezesha Serikali kujua idadi kamili ya raia wa Tanzania,raia wa nchi nyingine watakaokuwepo usiku wa kuamkia siku ya Sensa na wale wenye uraia wa nchi mbili. Aidha Serikali itaweza kujua mchanganuo wa raia waliopo katika nchi yetu.

18. Kwa kawaida unaishi Mkoa/Nchi gani?

Majibu ya swali hili yatasaidia kupata idadi ya watu waliopo katika kila Mkoa na hivyo kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo katika ngazi za Mikoa.

19. Je, kwa kawaida huwa unashinda wapi?

Swali linalenga kujua mahali ambapo mwanakaya anashinda au anapotumia muda wake mwingi wakati wa mchana.
Baadhi ya watu kwa kawaida huishi sehemu moja na kufanya kazi au kushinda sehemu nyingine kwa sababu mbalimbali.

Vilevile majibu ya swali hili yataisaidia Serikali kuboresha huduma katika maeneo ya mijini hasa nyakati za mchana na itasaidia kupata idadi ya watu walioko mijini wakati wa mchana (day population).

20. Je, ulizaliwa Mkoa/Nchi gani?

21. Je, ulikuja lini kuishi katika mkoa huu/nchini Tanzania?

22. Je, umeishi kwa muda gani katika mkoa huu/Nchini Tanzania?

23. Je, ulikuwa unaishi wapi kabla ya kuhamia hapa?

Maswali haya yataiwezesha serikali kujua namna watu wanavyohama na kuhamia kutoka sehemu moja hadi nyingine na kiwango cha ukuaji wa miji.

24. Je, ni ipi sababu kuu ya kuhamia mkoa huu/nchini Tanzania?

Majibu ya swali hili yatasaidia sekta ya uhamaji kujua sababu kuu inayowafanya watu kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

25. Je, ulikuwa unaishi Mkoa/Nchi gani wakati wa Sensa ya mwaka 2012?

Majibu ya swali hili yatasaidia kupima uhamaji wa muda mrefu.

26. Je, ulikuwa unaishi Mkoa/Nchi gani mwaka 2021?

Majibu ya swali hili yatawezesha kupima uhamaji wa muda mfupi.

27. Je, una vitambulisho vifuatavyo?
a. Cheti cha kuzaliwa
b. Tangazo la kuzaliwa
c. Hati ya kusafiria
d. Bima ya Afya ya Taifa/Mfuko wa Bima ya Afya wa Jamii (NHIF/CHF)
e. Bima nyingine ya afya

f. Kadi ya matibabu kwa wazee
28. Je, una nyaraka zifuatazo za kitaifa? (UMRI WA MIAKA 18 AU ZAIDI)
a. Kitambulisho cha Taifa (NIDA)
b. Namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA)
c. Kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi
d. Leseni ya udereva
e. Kadi ya kupiga kura
29. Tafadhali nitajie namba yako ya kitambulisho cha NIDA
30. Tafadhali nitajie namba yako ya kitambulisho cha Mzanzibar mkaazi
31. Je, una kitambulisho cha mjasiriamali?
32. Tafadhali nitajie namba yako ya kitambulisho cha Mjasiriamali

Maswali ya 28 hadi 32 yanalenga kujua aina mbalimbali ya vitambulisho walivyonavyo wanakaya. Majibu ya maswali haya yataiwezesha Serikali kupata idadi ya watu wote wenye vitambulisho na uhakiki wa vitambulisho hivyo.

Taarifa za namba za NIDA/Kitambulisho cha Mzanzibar Mkazi taarifa za mtanzania zinaweza kuunganishwa na kusaidia uboreshaji wa utoaji huduma za kijamii.

33. Je, baba mzazi wa [JINA] yuko hai?
34. Je, mama mzazi wa [JINA] yuko hai?

Swali la 33 na 34 yataulizwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18. Majibu ya swali hili yatatupa mwanga kuhusu idadi ya watoto yatima na hivyo kuiwezesha Serikali kupanga mipango na kutunga sera sahihi inayohusu watoto yatima.

B. SWALI LA 35 HADI 39 KWA WATU WOTE WENYE UMRI WA MIAKA 4 AU ZAIDI

35. Je, unajua kusoma na kuandika katika lugha ya Kiswahili, Kiingereza, Kiswahili na Kiingereza au lugha nyingine yoyote?

36. Je, unaweza kufanya hesabu rahisi za kujumlisha, kutoa, kugawanya na kuzidisha katika shughuli zako/zake za kila siku?

37. Je, kwa hivi sasa unasoma, uliachia, umemaliza au hujawahi kwenda shule?

38. Je, ni ipi ilikuwa sababu kuu ya kuacha/kutowahi kwenda shule?

39. Je, ni kiwango gani cha elimu ulichomaliza au uliachia au unachosoma kwa sasa?

Majibu ya maswali haya yataiwezesha Serikali kujua idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kufanya hesabu rahisi, ujuzi wa lugha tofauti, viwango vya elimu, waliomaliza, walioacha shule na sababu zipi zinazopelekea wanafunzi kuacha au kutokwenda shule. Aidha Serikali inaweza kutunga sera sahihi ya elimu kulingana na hali ilivyo

C. SWALI LA 40 HADI 61 KWA WENYE UMRI WA MIAKA 5 AU ZAIDI

40. Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, Je, ni kazi/shughuli gani ulitumia muda mwingi zaidi kuifanya?

41. Ingawa hukufanya shughuli yoyote wiki iliyopita, Je, unayo kazi ya kuajiriwa, shughuli katika shamba lako au katika biashara yako ambayo hukufanya wiki iliyopita na unatarajia kuendelea nayo?

42. Je, umefanya jitihada yoyote ya kutafuta kazi au shughuli katika kipindi cha wiki nne (4) zilizopita?

43. Je, Kwa sasa uko tayari kuanza kazi ya malipo au aina yoyote ya biashara, kilimo au kazi yoyote kama nafasi ikitokea?

44. Katika shughuli kuu, Je, ulikuwa/huwa unajishughulisha na nini?

45. Je, shughuli kuu unayofanya inamilikiwa na nani?

46. Je, ni ipi shughuli kuu ya kiuchumi katika biashara au mahali unapofanyia kazi?

Maswali ya 40 hadi 46 yanalenga kujua hali ya soko la ajira pamoja na shughuli za kichumi nchini. Majibu ya maswali haya yataiwezesha Serikali kujua ukubwa wa ajira katika sekta mbalimbali za uchumi, aina ya ajira, ukosefu wa ajira, nguvu kazi ya Taifa na sehemu walikoajiriwa au walikojiari.

47. Je, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita yaani kuanzia Agosti 2021 mpaka usiku wa kuamkia siku ya Sensa, ulifanya/alifanya kazi kama mchimbaji mdogo wa mchanga au madini yafuatayo?

48. Je katika kazi hii ya uchimbaji wa mchanga au madini [JINA] uliifanya/aliifanya kama nani?

Majibu ya swali la 47 na 48 yataiwezesha Serikali kuwatambua watu wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini ukijumuisha mchanga na kokoto.

Aidha, Serikali itatambua kwa uhakika hali ya ajira ya mwanakaya katika uchimbaji mdogo wa madini, iwapo ameajiriwa, amejiajiri au ni kibarua.

Taarifa hii itaisaidia Serikali kupanga mipango mahsusi kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo wa madini.

49. Je, katika mwaka wa kilimo wa 2021/22 umefanya shughuli za kilimo zifuatazo?
50. Je, ni aina gani ya Mazao?
51. Je, una haki gani ya umiliki wa ardhi uliyolima katika mwaka wa kilimo wa 2021/22?
52. Je, ni aina gani ya Mifugo unayofuga?
53. Je, ni aina gani ya Shughuli za Uvuvi, ukuzaji wa Viumbe Maji au kilimo cha mwani
unayojishughulisha nayo?
54. Je, ni aina gani ya shughuli za Misitu/Miti unayojishughulisha nayo?

Majibu ya maswali ya 49 hadi 54 yatasaidia kupata asilimia ya watu wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na Uvuvi pamoja na takwimu za viashiria vingine muhimu vya kilimo, mifugo na uvuvi kwa ajili uboreshaji wa sekta hiyo.

55. Je, unajishughulisha na shughuli ndogo ndogo zisizo rasmi/machinga?
56. Je, ni ipi shughuli kuu ya kiuchumi unayofanya?
57. Je, ni aina gani ya eneo ambalo unafanyia shughuli zako ndogo ndogo za ujasiriamali
zaidi?
58. Je, ni mwanachama wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA)?
59. Je, una mtaji wa shilingi ngapi na uliupata wapi?

Majibu ya maswali haya yataiwezesha serikali kuwatambua watu wanaojishughulisha na shughuli ndogo ndogo za ujasiriamali, aina ya shughuli wanazofanya, sehemu wanazofanyia biashara na mitaji waliyonayo.

Taarifa hizi zitasaidia kupanga mipango mbalimbali kwa ajili ya kuboresha biashara hizo ili ziweze kukua zaidi na kuajiri nguvu kazi kubwa zaidi, jambo ambalo litakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza kipato na kupunguza umaskini wa kipato.

Je, unamiliki ardhi kwa ajili ya kilimo au isiyo ya kilimo, binafsi au kwa pamoja na mtu mwingine?

61. Je, una hati ya umiliki wa ardhi yenye jina lako?

Majibu ya maswali ya 60 na 61 yataiwezesha Serikali kupata taarifa za watu wanaomiliki ardhi kwa jinsi na watu wenye hati za umiliki wa ardhi kwa ajili ya mipango ya kuendeleza sekta husika.

62. Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Je, ulimiliki au ulitumia vifaa vifuatavyo?
a. Simu janja/Kishikwambi
b. Simu ya kawaida
c. Kompyuta ya mezani (Desktop)
d. Kompyuta mpakato

63. Je, ulitumia kifaa hicho katika matumizi yapi?

Majibu ya maswali ya 62 hadi 63 yataiwezesha Serikali kupata taarifa za asilimia ya watu wanaomiliki na wanaotumia vifaa vya TEHAMA. Aidha, Serikali itaweza kupata taarifa za matumizi makuu ya vifaa hivyo vya TEHAMA kama vile kuwasiliana, kutafuta/kupokea taarifa kwa ajili kuboresha zaidi huduma hizo.

D. MASWALI YA 64 HADI 68 NI KWA WANAWAKE WENYE MIAKA 10 AU ZAIDI
64. Je, ulishawahi kuzaa watoto hai katika maisha yako/yake?

65. Je, umezaa watoto hai wangapi wa kiume na wangapi wa kike wanaoishi na wewe/yeye
katika kaya hii?

66. Je, umezaa watoto hai wangapi wa kiume na wangapi wa kike wanaoishi mahali pengine?
67. Je, umezaa watoto hai wangapi wa kiume na wangapi wa kike ambao kwa bahati mbaya
wamefariki?
68. Je, umezaa watoto hai wangapi wa kiume na wangapi wa kike katika kipindi cha miezi
12 iliyopita? (TAREHE 22 AGOSTI, 2022 KURUDI NYUMA HADI 23 AGOSTI, 2021)
(MIAKA 10 – 49).

Majibu ya maswali ya 64 hadi 68 yatawezesha kujua idadi ya watoto wanaozaliwa
hai kwa kila mwanamke na itawezesha kujua kiwango cha uzazi nchini kwa ajili ya
mipango ya maendeleo ya watu wake.

E. MAWALI YA 69 HADI 100 YANAHUSU KAYA KWA UJUMLA WAKE

69. Je, kuna kifo chochote kilichotokea katika kaya hii katika kipindi cha miezi 12 iliyopita?
(TAREHE 22 AGOSTI 2022 KURUDI NYUMA HADI 23 AGOSTI 2021)

70. Je, ni watu wangapi walifariki katika kipindi cha miezi 12 iliyopita?
71. Je, aliyefariki alikuwa mwanaume au mwanamke?
72. Alifariki akiwa na umri wa miaka mingapi?
73. Je, ni nini ilikuwa sababu kuu ya kifo?

Maswali ya 69 hadi 73 yanalenga kupata kiwango cha vifo, vifo vitokanavyo na uzazi na sababu nyingine za vifo. Hali kadhalika kupata wastani wa umri wa kuishi (life expectancy).

Majibu ya swali hili yatawezesha kupata taarifa za vifo katika kaya katika kipindi husika.

F. SWALI LA 74 HADI 77 IWAPO ALIYEFARIKI NI MWANAMKE
74. Je, kifo kilitokea wakati wa ujauzito?
75. Je, alifariki wakati wa kujifungua?
76. Je, alifariki ndani ya kipindi cha wiki 6 baada ya ukomo wa mimba, bila kujali mimba ilivyofikia ukomo wake (mimba kutolewa/kuharibika/kujifungua)?

77. Je, kifo hiki kilitokea kwenye kituo cha kutolea huduma ya afya, nyumbani au njiani?

Majibu ya maswali ya 74 hadi 77 yataiwezesha Serikali kupata kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi. Aidha kufahamu vifo hivyo vilitokea wapi zaidi; nyumbani, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya au njiani kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuimarisha huduma za afya.

78. Je, nini hali ya umiliki wa jengo kuu linalotumiwa na kaya hii?
79. Je, una haki gani ya kisheria juu ya umiliki wa ardhi ulipojenga/alipojenga nyumba hii?
8
80. Je, sehemu kubwa ya nyumba kuu inayotumiwa na kaya hii imeezekwa na nini?
81. Je, sehemu kubwa ya nyumba kuu inayotumiwa na kaya hii imesakafiwa na nini?
82. Je, sehemu kubwa ya kuta za nyumba kuu inayotumiwa na kaya hii imejengwa na nini?

Majibu ya maswali ya 78 hadi 82 yataisaidia Serikali kujua hali ya umiliki wa nyumba ya kaya, hali za nyumba wanazoishi watu, ubora wa vifaa vilivyotumika katika ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya nyumba.

83. Je, kaya hii ina vyumba vingapi vinavyotumika kwa kulala?

Lengo la swali hili ni kuangalia msongamano wa watu katika kaya husika na hutumika katika kuweka Sera za kuboresha maisha ya watu na afya zao.

84. Je, ni nini chanzo kikuu cha maji ya kunywa katika kaya hii?
85. Je, ni nini chanzo kikuu cha nishati inayotumiwa na kaya hii kwa kupikia?
86. Je, ni nini chanzo kikuu cha nishati kinachotumiwa na kaya hii kwa kuangazia?
87. Je, kaya yako inatumia choo cha aina gani?

Majibu ya swali namba 84 hadi 87 yataiwezesha Serikali kujua hali ya makazi ya
wanachi na nishati zinazotumika kwa kuangazia, na kupikia.

88. Je, ni njia gani kuu inayotumiwa na kaya yako kutupa taka ngumu?
89. Je, taka kwenye kaya yako zinakusanywa na mamlaka ipi?
90. Je, kaya yako ina utaratibu wa kutenganisha taka za kutoka jikoni, taka za plastiki, taka
za glasi, taka za chuma na taka za kielektroniki?
91. Je, ni njia gani kuu inayotumiwa na kaya yako kutupa taka za kieletroniki?

Majibu ya maswali namba 88 hadi 91 yataiwezesha Serikali kupanga mipango madhubuti ya kuimarisha mazingira bora ya utupaji wa taka katika maeneo wanayoishi watu kwa ajili ya uboreshaji na uhifadhi wa mazingira.
92. Je, kaya yako inamiliki vifaa/rasilimali zifuatazo?

Majibu ya swali hili litawezesha kupata taarifa za kukokotoa kiashiria cha umasikini usio wa kipato na kuweka mikakati ya kuboresha maisha ya watu.

93. Je, kaya hii ilitumia ardhi kwa uzalishaji wa mazao katika mwaka wa kilimo 2021/22?
94. Je, kaya hii ilifuga au ilitunza ng'ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, punda au kuku kwa
mwaka wa kilimo 2021/22?

95. Tafadhali, nitajie idadi ya ng'ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, punda au kuku, kama ilivyokuwa katika usiku wa kuamkia siku ya Sensa

96. Je, kaya hii inatumia aina gani kuu ya ufugaji?

97. Katika kipindi cha mwaka wa kilimo 2021/22, Je, kaya hii ilijishughulisha na kilimo cha miti ya kupanda?

98. Je, kuna mwanakaya yeyote katika kaya hii anajishughulisha na ufugaji wa nyuki?
Majibu ya maswali namba 93 hadi 98 yataisaidia serikali kujua idadi ya kaya zinazojishughulisha na kilimo,ufugaji wa mifugo kwa aina ya mifugo, kilimo cha miti na ufugaji wa nyuki na hivyo kuweza kuboresha sera zinazohusu sekta hiyo.

99. Je, kaya hii ina Anwani ya Makazi?
100. Tafadhali nitajie namba ya Anwani ya Makazi na Jina la Barabara/Kitongoji

Majibu ya maswali namba 104 hadi 106 yatasaidia Serikali kuhakiki namba za anwani za Makazi kama zilivyosajiliwa katika zoezi la usajili wa anwani za makazi pamoja na jina la barabara/mtaa/Kitongoji ilipo kaya husika. Taarifa
zitakazokusanywa zitasaidia kufahamu maeneo ambayo hayana anwani za makazi na kuweka mikakati ya kukamilisha au kuboresha huduma hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news