NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Japan imeahidi kutoa dola za Marekani bilioni 30 ili kuziwezesha nchi za Afrika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuimarisha utunzaji wa mazingira.
Akizungumza kwa njia ya mitandao wakuu hao kwenye ukumbi wa Palais des Congres, jijini Tunis, Waziri Mkuu Kishida alisema kiasi hicho cha dola bilioni 30 kitatolewa kwa kipindi cha miaka mitatu ili kuimarisha utunzaji wa mazingira, uwekezaji hasa kwa vijana, sekta za afya, viwanda na elimu.
“Ijapokuwa siko pamoja nanyi kwenye mkutano huo, bado dhamiri yangu ya kuendeleza bara la Afrika iko palepale, haijabadilika. Kwa kuanzia, Japan itaanzisha "Japan’s Green Growth Initiative with Africa" ambapo itatoa dola za Marekani bilioni nne kwa taasisi za umma na za binafsi barani Afrika ili kuziwezesha kutekeleza mpango huo,” alisema.
Alisema Japan imelenga kukuza uwekezaji ambapo safari hii wamelenga kuwainua vijana. Katika awamu hii, alisema watawalenga zaidi vijana wanaoanzisha makampuni na hatua hiyo itawapa fursa vijana wa Afrika na wa Japan kufanya kazi kwa karibu.
Kuhusu kuboresha maisha ya Waafrika, Mhe. Kishida alisema kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) watatoa dola za Marekani bilioni tano ambazo zinajumuisha mkopo mpya wa dola za Marekani bilioni moja zinazolenga kuzisaidia nchi hizo kumudu madeni.
Waziri Mkuu huyo alisema kujitokeza kwa janga la corona kumetoa funzo kuwa kuna haja ya kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Na kwa kuzingatia hilo, Serikali yake itachangia kiasi dola za Marekani bilioni 1.08 ili kuiwezesha Afrika kukabiliana na UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria na kuimarisha mifumo ya afya.
“Vilevile, tutaimarisha rasilmali watu kwa kuwajengea uwezo wataalamu barani Afrika. Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Japan inatarajia kuwajengea uwezo zaidi ya watu 300,000 kutoka bara la Afrika katika sekta za viwanda, afya, utabibu, elimu, kilimo, sheria na utawala.”
Kuhusu kilimo, alisema hivi karibuni Japan kwa kushirikiana na AfDB imeamua kutoa dola za marekani milioni 300 ili kuzisaidia nchi za Afrika kuzalisha chakula kwa wingi na kuwajengea uwezo watu 200,000 walioko kwenye sekta ya kilimo. Aidha watatoa msaada wa chakula wenye thamani ya dola za marekani milioni 130 ili kuzisaidia nchi hiyo kukabiliana na upungufu wa chakula.
Mapema, akifungua mkutano huo, Rais wa Tunisia, Mhe. Kais Saied ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano wa TICAD 8 alisema nchi za Afrika zina rasilmali nyingi lakini watu wake bado wanakabiliwa na umaskini.
“Kupitia kikao hiki, tuangalie tunaweza vipi kutumia rasilmali hizo ili kuondokana na umaskini kwa watu wetu. Hili si suala la nchi moja tu, bali ni letu wote. Na katika hatua hii, inabidi tuje na njia mpya ya kutuwezesha kusonga mbele na zaidi tuwe na ushirikiano wa kisiasa ulio imara,” alisema.
Naye Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Macky Sall ambaye pia alitoa hotuba ya ufunguzi sambamba na Waziri Mkuu wa Japan, alisema bara la Afrika linahitaji kuwezeshwa kuwa na nishati ya uhakika ili liweze kuzalisha bidhaa zake.
“Tunahitaji kuona nchi za Kiafrika zikizalisha mbolea ya kutosha ili tuwe na uhakika wa kilimo, kwa hiyo tunakaribisha wabia kutoka Japan katika sekta hii muhimu ya uzalishaji katika nchi nyingi,” alisema.
Kuhusu amani, alisema uwepo wa amani ni mada ambayo haihitaji mjadala na kitu muhimu kwa ukuaji na maendeleo barani Afrika. “Kupitia mkutano wa nane wa TICAD, na kupitia ubia, tunaweza kupata maendeleo ya uhakika na endelevu,” alisema.
Kaulimbiu ya mkutano wa nane wa TICAD ambao umehudhuriwa na washiriki 3,000 kutoka nchi za Afrika na mashirika ya kimataifa ni: “Kukuza Maendeleo Endelevu ya Afrika kwa ajili ya Waafrika” (Promoting Africa-led, Africa-owned Sustainable Development).