NA ADELADIUS MAKWEGA
IJUMAA ya Agosti 5, 2022 nilifika katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) mkoani Dodoma iliyo katikati ya jiji hili kwenda kuomba kitambulisho kipya kwani kile cha zamani kilipotea.
Nilipofika katika ofisi hii ya umma, nilipokelewa vizuri sana na foleni ndefu ya wateja wa ofisi hii waliojaa katika mabenchi manne, huku mabenchi matatu yaliyokuwa katika umbo la U, umbo hili likinikumbusha nilipokuwa nasoma shule ya msingi wakati ule zile voweli a,e, i ,o na u na namna mwalimu wangu wa darasa hilo alivyokuwa akizirekebisha herufi zile nilizoziandika zikiwa zinapiga tikitaka.Huku benchi lingine lililokuwa njiani ambalo liliwakaribisha wageni.
Mandhari ya ofisi hii iliyo na vyumba kadhaa ambapo vyumba vitatu niliweza kuviona kwa macho yangu, chumba nambari moja kilikuwa na maafisa wawili ambao walipokea maombi mbalimbali, huku wakifanya kazi vizuri sana, hasa hasa kijana mmoja ambaye alionekana kufanya kazi kwa kujituma mno, akijitahidi kuipunguza foleni, meza yake ilikuwa mlangoni katika ofisi hii punde ukifungua mlango wa ofisi hii.
“Haya jamani ingieni watano watano, hakikisheni mnaheshimu foleni yetu, sawa jamani?” Kijana huyu alituambia wateja wake kwa lugha ya ukarimu.
Chumba nambari 2 ni chumba cha kupiga picha za Biometric ambapo hapa palikuwepo na kijana mmoja mpole sana, mchapa kazi mno na yeye akijaribu pia kupambana na foleni ndefu ya wateja wa NIDA waliokuwa wanatamani kuingia katika chumba chake, lakini wateja hao walitumia hata saa mbili mtu kufika hapo na kuingia katika ofisi hii.
Shida kubwa ikiwa mtandao.Kijana huyu nilimuona amesimama muda wote tangu nilipofika hapo, macho yangu hayakujaliwa kumuona ameketi, japokuwa kiti kilikuwepo. Kwa hakika kiti chake nadhani kipo likizo ya kukaliwa kwa muda mrefu.
Chumba cha tatu kilipewa maandishi (scanning) humo kulikuwa na jamaa ambao walikuwa wanapiga soga tu, ambao hawakuona wala kujali foleni hii ya wadau wao kama ni kero kwao, binafsi sikujaliwa kuwafahamu kama walikuwa watumishi wa NIDA au wageni.
Niliingia na kupata huduma katika ofisi nambari moja na kueleza shida yangu, huyu kijana mchapakazi akiniambia kuwa kwa utaratibu wa sasa wale wote waliojiandikisha zamani wakija hapa wanatakiwa kuchukua fomu nambari 1A ambayo imepewa jina la FOMU YA UTAMBULISHO. Jambo hilo lilinishangaza mno mbona nilikamilisha taratibu zote iweje NIDA wanijazishe nijaze fomu nyengine?.
“Wateja wetu wapya wanajaza fomu hii, lakini nyie mliojiandikiswa wakati ule fomu hii haikuwepo, ndiyo maana mnaijaza sasa punde mkija hapa.”
Nikasema sawa, nilitakiwa kulipa shilingi 20,000 halafu nikapewa fomu hiyo na kisha kwenda kwa Afisa Mtendaji wa Kata na Afisa Uhamiaji wa Wilaya ndipo niirudishe tena NIDA, mwanakwetu nilifanya hivyo.
Nilipokwenda kwa mtendaji wa kata aliijaza vizuri na kugonga muhuri halafu kwenda kwa Afisa uhamiaji na yeye aliweka sahihi na kugonga muhuri na mimi kurudi NIDA.
Nilirudi ofisi nambari moja kwa kijana hodari na kusema kuwa sasa mzee umekamilisha kazi hii nenda ofisi nambari mbili kwa jamaa wa Biometric. Nilifika hapo na kumkabidhi kijana huyu na yeye kuisoma vizuri na kuingiza baadhi ya takwimu katika kompyuta yake.
“Hapa mambo yamekamilika kitambulisho chako kitapatikana baada ya miezi mitatu.” Wakati ninatoka katika ofisi hii nikakutana na Devota Ntisi huyu ni afisa msajili wa NIDA ambaye ni rafiki yangu wa miaka mingi, nilizungumza naye na kupiga naye picha kidogo.
Msomaji wangu fahamu kuwa Devota Ntisi yeye ni Mrangi wa Kondoa mkoani Dodoma, usihisi kuwa mwanakwetu amepata jiko jipya huku Dodoma, la hasha, huyu ni dada yangu tena ni dada rafiki, lakini mwenye dada hakosi shemeji. Mwanakwetu, hautakiwi kumuonea wivu dada yako, maana haramu kwako halali kwa wengine.
Niliingia katika basi la kwenda kwetu huko madongo poromoka nilijiuliza maswali mengi, mojawapo nini ni umuhimu wa NIDA wa kuiongoza fomu namba 1 A kujazwa kwa siye tuliojisajili zamani, ina maana gani?
Mbona inakuwa kama fomu ya kuongeza urasimu tu, kwa nini tena inaturudisha kwa Uhamiaji na kwa Mtendaji wa Kata? Nilisema moyoni NIDA inapaswa kuwa na wivu wa kiutendaji kwa kuyamaliza mambo yake yenyewe bila ya kuzishirikisha taasisi zingine kama hakuna shida.
NIDA imekuwa inatumia muda mrefu mno kuwapatia kadi hizo wateja wake, mathalani kama nilivyoambiwa mimi nirudi baada ya miezi mitatu, maana yake Agosti, ipite Septemba itapita, Oktoba hivyo hivyo hadi Novemba mwanzoni.
Mwanakwetu miezi mitatu ni mingi mno, hapo kwa mkulima kama mimi ninapanda mahindi na ninayavuna, huku bado NIDA hawajanipa kadi yangu.
Hapo mtu anaweza akaomba kadi ya NIDA akaumwa, akafa na akazikwa kadi haijatoka, hilo halikubaliki kabisa.`Mkurugenzi Mkuu wa NIDA ndugu yetu Esmaily Rumatila jitahidi kadi zetu zipatikane kwa haraka.
Ndugu yetu Rumatila afahamu kuwa kadi za NIDA siyo uchawi zinapaswa kutolewa kwa haraka kwa wale wote waliotimiza vigezo hivyo, hilo litaiongezea mamlaka hii hata mapato.
Kumekuwa na hoja ya kuwepo kwa muda wa kuisha kwa kadi (expire date) hoja hii itakubalika tu kama NIDA yenyewe itagharamia gharama za kadi zitakazotolewa baada ya kuhuhisha na siyo waombaji, natambua kuwa ni haki ya waombaji kulipia kadi hiyo kama imeharibika au kupotea hapo hakuna shida na siyo vinginevyo.
Msomaji wangu kumbuka tu nipo katika hiace ya Sabasaba-Chamwino Ikulu, nikapatwa na usingizi mzito, mara baada ya muda kidogo nikasikia kondakta akinadi, Njiapanda ya Chamwino ! Njiapanda ya Chamwino! Njia Panda ya Chamwino, mwanakwetu nikashituka, ah nikajua kumbe sasa ninakaribia kituo cha kwangu nikaweka vifurushi vyangu vizuri na kujiandaa kushuka kituoni changu.
makwadeladius@gmail.com
0717649257