NA GODFREY NNKO
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewahakikishia wadau wa habari kuwa, Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Habari nchini hayatapelekwa bungeni bila pande zote kukubaliana na kuridhika.
Hayo yamesemwa Agosti 26, 2022 na Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye katika mjadala wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC ambao uliangazia kuhusu mapendekezo hayo.
"Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.
"Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho.
"Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane.
"Kwa hiyo tutakwenda, tutazungumza. Na mimi nina hakika kwamba tutakubaliana na spirit iliyopo ni nzuri, Serikali tupo tayari kuondoa baadhi ya vifungu, kwa sababu hatuna nia mbaya.Lakini pia Jukwaa la Wahariri na wadau wa habari kwa spirit ambayo ninaiona wapo pia tayari kukubaliana baadhi ya mambo. Kwa hiyo twende tukashawishiane,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Nape.
Amefafanua kuwa, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa ujumla wake imelenga kutatua matatizo,"na haya matatizo pande zote mbili tunakubaliana, Serikali na wanahabari,kwa mfano tuna tatizo la kwamba leo mwanahabari akikosea, kinaadhibiwa chombo kizima cha habari, tofauti na ilivyo taaluma nyingine kama udaktari.
"Tunasema tunalitatuaje hilo tatizo,sisi tukasema tumpe leseni huyu mwandishi ili akikosea aadhibiwe binafsi, wenzetu wakasema hili la leseni limekaa vibaya, sisi tukasema sawa, tuwekeeni mezani nini mnadhani kimekaa vizuri, halafu tutashauriana tutafika mahali tutakubaliana.
"Kwa sababu lengo letu ni kutatua changamoto ambazo tunaziona, kwa hiyo Serikali ipo tayari, kikao cha kwanza kimeenda vizuri na nimeridhika,sasa tutakwenda kikao cha pili ambacho nitalazimika kwenda mwenyewe tukae pamoja tuzungumze tujenge hoja, wanawaza nini, tunawaza nini mwishowe tutakubaliana, nchi ni yetu wote,"amesema Mheshimiwa Nape.
Kwa nyakati tofauti wadau wa habari wakiwemo wananchi wameieleza DIRAMAKINI kuwa, kauli ya Mheshimiwa Waziri Nape kwamba hawataenda bungeni hadi wakae pamoja wakubaliane na pande zote kwa maana ya Serikali na wadau wa habari inadhirisha ni kwa namna gani Serikali ya Awamu ya Sita inavyothamini na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
"Mheshimiwa Waziri Nape ametoa maneno ya faraja sana, yanatupa nguvu, si sisi wananchi tu, bali kwa taasisi za habari ambazo kwa namna moja au nyingine tunaamini itajenga na kuimarisha umoja ambao utawezesha sisi wananchi kupata taarifa nzuri na za kichunguzi ambazo zitaleta majawabu ya changamoto zinazotukabili,"amesema Herman Julius mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mei 2,202 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alielekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru vya vyombo vya habari nchini zirekebishwe.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti' katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.
“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia.
Rais Samia pia alishauri waandishi wa habari kuwa wazalendo kwa kuandika mambo mazuri ya kutetea Bara la Afrika huku akiwataka waandishi wa habari kuzitangaza mila na desturi nzuri za Tanzania.
“Tunazo mila na desturi tunapaswa kuzilinda, na nyinyi waandishi wa habari mnatakiwa kuzilinda ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu. Baadhi ya watu wanaposti picha chafu mtandaoni, wanajianika mtandaoni, wengine wanafanya hivyo kwa kutojua madhara ya kufanya hivyo,"alisema Rais Samia.