Konga:Maboresho ya kihuduma NHIF yanalenga kumlinda mwanachama na sio kumwadhibu

NA DIRAMAKINI

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umesema kuwa maboresho na udhibiti wowote unaofanywa na Mfuko huo ni kwa nia njema ya kumlinda na sio kumwadhibu mwanachama wake.

Aidha, imeelezwa kuwa mfuko una wajibu wa kuhakikisha unalinda uhai wake, ubora wa huduma anazopata mwanachama ili kuepukana na matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na kutolewa kwa huduma kiholela.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari Jijini Dar es Salaam leo.

"Control tunazoziweka hazina maana ya kumuumiza mwanachama wetu, kama Mfuko tunao wajibu wa kulinda na kuhakikisha ubora wa huduma anazopata mwanachama wetu kulingana ni miongozo ya tiba iliyipo, mfano dawa zikitumika vibaya ni sumu hivyo udhibiti tunaoufanya ni kwa maslahi makubwa ya mwanachama wetu," alisema Bw. Konga.

Alitolea mfano wa udhibiti katika baadhi ya vipimo na akaweka wazi kuwa katika eneo hilo takwimu zilionesha namna vipimo vilivyokuwa vikitumika vibaya kabla ya kuweka udhibiti katika mifumo.

"Nitoe mfano wa eneo moja tu la kipimo cha MRI kabla ya kuweka udhibiti vipimo vilifanyika kwa idadi kubwa na baada ya kuweka udhibiti wa mifumo kulingana na miongozo ha tiba vilipungua kutoka 800 hadi 400 kwa mwezi," alisema Bw.Konga.

Kutokana na hilo niweke wazi kuwa Mfuko utafanya maboresho yake kwa kuzingatia uhalisia na miongozo ya Afya iliyopo nchini.

Akizungumzia suala la gharama za matibabu, amesema kuwa mfuko unao wajibu wa kuhakikisha unaweka gharama zake kwa kuzingatia hali halisi ili kuepuka kusababisha mfumuko wa gharama katika eneo la matibabu na kuleta changamoto kwa wananchi.

"Zipo huduma ambazo awali hapa nchini hazikupatikana kwa wingi na gharama zake zilikuwa juu sana lakini kwa sasa zipo kwa wingi na gharama kwenye soko imeshuka hivyo ni muhimu kufanya mabadiliko hayo, huduma hizo ni pamoja na za kusafisha damu, dawa za kansa na huduma nyingi za kitalaam," alisema Bw. Konga.

Ili kwenda na uhalisia wa soko, alisema kuwa Sheria inautaka Mfuko kutoa taarifa kwa Watoa huduma wenye mkataba na NHIF za mabadiliko ya bei za huduma za matibabu kwa muda wa siku 90 na tayari Mfuko umeshatoa taarifa hiyo na katika kipindi hicho hadi kufikia Novemba Mosi mwaka huu Mfuko utakutana na kujadili na wadau wake mabadiliko hayo kabla ya kuanza kuyatekeleza.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwahakikishia wanachama kuwa Mfuko iko imara na una fedha za kutosha kuwahudumia na mkakati uliopo sasa ni wa kufikia wananchi wengi zaidi ili kusaidia kuuimarisha zaidi kwa kuwa wingi wa wanachama huwezesha Mfuko kuongeza wigo wa huduma kwa wanachama wake .

Mkutano na vyombo vya habari ni moja ya mikutano ya wadau iliyopangwa na mfuko ili kutoa elimu juu ya maboresho yanayofanywa na sababu zake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news