Makamu wa Pili wa Rais:Milango ya uwekezaji Zanzibar ipo wazi

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema milango ya uwekezaji iko wazi kwa Wawekezaji, kuwekeza katika Sekta ya Nishati, hasa Mafuta na Gesi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi ya Kongamano la Nne la Kimataifa la Nishati lililofanyika jijini Dar es salaam kwa siku mbili, Agosti 3 na 4, 2022. Watatu waliokaa ni Waziri wa Nishati, January Makamba, na aliyesimama nyuma ya Makamu wa Pili wa Rais, ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Kheri Mahimbali. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah amesema hayo wakati akifunga Kongamano la Nne la Kimataifa la Nishati lililofanyika jijini Dar es salaam kwa siku mbili, Agosti 3 na 4, 2022.

Abdullah alisema kuwa, makapuni mengi makubwa yameshiriki katika kongamano hilo kubwa, na Zanzibar imekwisha kufungua milango ya uwekezaji kwa makampuni na wadau mbalimbali wa sekta ya Nishati kuwekeza Zanzibar.

Ameweka wazi kuwa Serikali iko tayari kwa mazungumzo ya uwekezaji kwa Kampuni ya aina yeyote ambayo iko tayari kuwekeza Zanzibar katika sekta ya nishati hasa mafuta na gesi kwa maslahi pande zote mbili ambazo ni serikali na wananchi wake pamoja na muwekezaji husika.
Kwa sasa serikali ya Zanzibar imepiga hatua kubwa katika sekta ya Mafuta na Gesi hivyo kampuni za uwekezaji zinakaribishwa ili kutekeleza miradi ambayo imebainika.

“Kongamano hili kubwa limefungua milango na kuongeza fursa zaidi za uwekezaji kwa nchi yetu, kwani wawekezaji walioshiriki katika kongamano hili wamefahamishwa juu ya fursa zilizopo kwa upande wa Tanzania Bara na pia Zanzibar, hivyo waje tuzungumze katika masuala ya uchimbaji wa mafuta au ufuatiliaji wa miradi mingine kwa maslahi ya pande zote mbili,” alisisitiza Abdullah

Ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau wengine katika kuandaa na kufanikisha kongamano hilo kubwa lililowakutanisha kwa pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya nishati, ikiwepo makampuni makubwa zaidi ya 80.
Mhandisi Mkuu wa Mafuta na Gesi , Joyce Kisamo ( katikati) na Mhandisi Anita Ringia(kulia) wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah wakati akifunga Kongamano la Nne la Kimataifa la Nishati lililofanyika jijini Dar es salaam kwa siku mbili.

Alisema kongamano hilo ni litaongeza chachu kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika nyanja mbalimbali za maendeleo hasa katika sekta ya nishati, ili kuinua uchumi wa nchi yetu kwa kuwa nishati ni nguzo muhimu katika maendeleo ya nchi yeyote duniani.

Aidha aliishauri Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali kuwa ikiwapendeza kongamano kama hilo lifanyike Zanzibar ili kutoa nafasi zaidi kwa Zanzibar kutangaza fursa zilizopo.
Mkujrugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Nishati, Petro Lyatuu, (kushoto) Katibu wa Naibu Waziri wa Nishati, Ngeleja Mgejwa (katikati) na Mjilojia Mwandamizi wizara ya Nishati Jacob Mayala(kulia) wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah wakati akifunga Kongamano la Nne la Kimataifa la Nishati lililofanyika jijini Dar es salaam kwa siku mbili.

Aidha alisema kuwa muitikio mkubwa wa washiriki katika kongamano hilo kutoka maeneo mbalimbali dunani, ni matokeo ya ziara za Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi kutembelea nchi na makampuni makubwa mbalimbali duniani na kufanya nayo mazungumzo ya kutangaza fursa zilizopo nchini.

Vilevile aliwataka waandishi wa habari kutumia vyema kalamu zao kuhabarisha umma wa Tanzania na hata nje ya Tanzania mambo mazuri yanayotokea nchini kama walivyotangaza kongamano hilo.

Pia wawe wazalendo katika kutekeleza majukumu yao kwa nchi yao kwakuwa wao ni watu muhimu katika kufikisha taarifa kwa maslahi ya taifa letu.

Kando ya Kongamano hilo, Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) limesaini makubaliano ya kuendeleza Mradi wa Nishati Jadidifu na Kampuni ya Masdar inayomilikiwa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E).

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Waziri wa Nishati January Makamba, alisema kuwa makubaliano hayo ni matunda ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya mapema mwaka huu katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E).
Waziri wa Nishati, January Makamba( wa pili kulia) akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya kuendeleza Mradi wa Nishati Jadidifu na Kampuni ya Masdar inayomilikiwa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E), Agosti 4, 2022 jijni Dar es salaam. 

Alisema utekelezaji wa makubaliano ya miradi hiyo utafanyika kwa awamu mbalimbali kwa lengo la kuzalisha hadi kufikia Megawati 2000 za umeme Jua nchini.

Alisema utekelezaji wa mkataba huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Uendelezaji wa Biashara na Uwekezaji wa Masdar, Abdullah Zayed alisema kuwa miradi iliyopo katika makubalino hayo, uendelezaji wake unategemea kufikia Megawati 5000 kufikia mwaka 2025.

Katika kongamano hilo, wataalam kutoka Wizara ya Nishati waliwasilisha mada kuhusu maendeleo ya sekta ya nishati nchini, pia ushiriki wa wahandisi wanawake katika nafasi za uongozi hasa katika sekta ya nishati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news