NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw.Theophil Makunga amesema kuwa, uundaji wa Baraza Huru la Vyombo vya Habari ni moja wapo ya tiba kuu ya changamoto inazokumbana nazo tasnia hiyo nchini.

“Maombi yetu ni kwamba, ile Idara ya Habari Maelezo ibadilishwe jukumu lile, badala ya mambo yanayohusu tasnia ya habari kupewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, lipewe Baraza Huru la Vyombo vya Habari kusimamia,” amesema Makunga.
Ameeleza kuwa, Baraza Huru la Vyombo vya Habari Huru linapaswa kuwa kama mabaraza ya taaluma zingine akitoa mfano wa namna Baraza la Madaktari na Baraza la Wanasheria yanavyoendeshwa.
“Kinapaswa kuwa chombo cha wanataaluma wahusika kinachoendeshwa na waandishi wa habari. Kwa hiyo, matatizo yote yatakayokuwa yanahusu taaluma ya waandishi wa habari, yapitie kule kwenye lile baraza ambalo litakuwa likiendeshwa na waandishi wa habari wenyewe,"amesema.
Hata hivyo, Makunga ameipongeza Serikali kwa kufungua mlango wa majadiliano kuhusu mabadilio ya sheria zinazoongoza tasnia ya habari nchini.
Kwenye kipindi hicho, Makunga amesema serikali imeona umuhimu wa kufungua mjadala wa mazungumzo ya sheria hizo, kutokana na wadau wa habari kueleza kuwepo haja ya kuzipitia upya.
Aidha,tayari Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeandaa mkutano wa wadau wa habari utakaofanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 11 hadi 12,2022.
“Kuna vipengele vinatubana, tunaishukuru Serikali kwa kukubali kufungua mjadala wa mazungumzo yanayolenga kuangalia namna gani ya kuondoa hivyo vipengele ili tuwe huru zaidi,” amesema Makunga.

“Sheria hii ilikuwa ikiongoza uandishi wa habari, utangazaji na namna gani ya kufanya, ilikuwa inasema ukiwa na kosa kwenye gazeti, anaweza kushtakiwa mwandishi, mhariri, mmiliki, mchapaji wa gazeti,” amesema.
Hata hivyo anasema, kutokana na mabadiliko ya teknolojia, sheria sasa inapaswa kuendana na wakati uliopo.