NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Benki ya NMB Plc wamesaini Hati ya Makubaliano ya kutengeneza Mfumo wa Kidigitali wa kutunza taarifa za Diaspora, (Diaspora Digital Hub).
Makubaliano hayo yamesainiwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora Balozi James Bwana kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine na Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB Bw. Alfred Shao kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa benki ya NMB katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Akiongea katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Balozi Bwana amesema mfumo huo wa kidigitali utaisaidia Serikali kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha Diaspora wa Tanzania waliopo sehemu mbalimbali ulimwenguni kupata huduma mbalimbali na kushiriki kidigitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo, biashara, uchumi na uwekezaji.
“Ushirikiano wa Wizara na Benki ya NMB Plc ni wa muda mrefu na wenye mafanikio mengi katika kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya Tanzania. Wizara ina imani kuwa kupitia udhamini huu wa shilingi milioni 100 kutoka Benki ya NMB zitawezesha kukamilisha matengenezo ya mfumo wa Diaspora Digital Hub na hivyo kuboresha huduma mbalimbali zenye kukidhi mahitaji ya Diaspora kote ulimwenguni,” amesema Balozi Bwana.
Balozi Bwana ameongeza kuwa, mfumo huo pamoja na mambo mengine, utafungua uwezekano wa fursa zaidi za ushirikiano kati ya Wizara na Benki hiyo ya NMB utawezesha utunzaji wa taarifa mbalimbali za Diaspora wa Tanzania popote walipo ulimwenguni na hivyo kurahisisha kazi ya uratibu wa Diaspora.
Balozi Bwana amesema ni mategemeo ya Serikali kukamilika kwa mfumo huo kutaweza kuwatambua,kuwasajili na kuwawezesha Diaspora wa Tanzania Duniani kote kupata huduma nyingi na muhimu wanazohitaji na kushiriki kidijitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo biashara, uchumi na uwekezaji hapa nchini.