NA DIRAMAKINI
KUNDI la Muziki wa dansi la Orchestra Sikinde Original, Jumatatu hii linaachia wimbo wake wa pili mpya uitwao MCHEPUKO maarufu kama "NYUMBANI KUMENOGA".

Mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Fatuma Munene amesema wimbo huo unazungumzia Kisa cha wanandoa ambao hawakuwa sawa na kuangukia kwa mchepuko ambapo Bado mambo hayakuwa sawa hadi pale mwenza anapomwambia mwenzie arudi nyumbani Kumenoga.
Munene alisema Sikinde Original ina lengo la kurejesha ladha ile ya Sikinde ya miaka ya nyuma ikachanganya na vionjo vya kisasa.
"Kuna wanamuziki wengi waliopita Sikinde watatumika katika kutengeneza albamu ya kundi hili na katika albamu wimbo wa kwanza ni Mchepuko....huko mbele zipo suprise nyingi sana, tujachojaribu kufanya ni kuinua muziki wa dansi ambao wapo wanaosema umeshuka,"

Kwa upande wa ala magitaa yamepigwa manne ambapo Solo limepigwa na Omary Seseme, Second Solo, Mkongwe Abdalah Gama, rythim Mjusi Shemboza wakati Bass ni Bonny Chande.
Juma Choka ameshiriki kwenye Drums huku Ibrahim Chande kwenye Trumpet. Huu ni wimbo wa pili kutolewa na Orchestra Sikinde Original. Wimbo wa kwanza ni Sensa ambao ni maalum kuhamasisha zoezi la kuhesabiwa. Video ya Mchepuko iko mbioni kuachiwa pia.