NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Bw.Nehemiah Mchechu amesema kuwa, shirika hilo linaamini wawekezaji ni wadau muhimu kwa ustawi bora wa uchumi wa Tanzania na kufungua fursa za ajira kwa Watanzania.
Ameyasema hayo Agosti 11, 2022 jijini Dar es Salaam baada ya kujumuika na Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini waliopo hapa nchini.
Wafanyabiashara kupitia jukwaa hilo,wameonesha nia ya kuwekeza katika Sekta ya Nyumba nchini ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka msisitizo mkubwa katika uwekezaji.
Mheshimiwa Rais anasisitiza kuwa, sekta binafsi ndiyo itafanya biashara na serikali itabakia kusimamia sera za kuwajengea mazingira rafiki wawekezaji hao ikizingatiwa kuwa, hapa nchini kuna fursa muhimu za kibiashara ikiwemo utawala bora.
"Tunaamini wawekezaji ni muhimu sana, na sisi tunatembea katika mapito ya Royal Tour kwa kutangaza fursa na kuwaleta wawekezaji na National Housing tuna mikakati mipya sasa hivi, ambayo tumeipanga 'of course' tutawajuza karibuni.
Pia Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa,shirika hilo limejiwekea malengo ya kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Nyumba nchini.
"Tunaamini kwamba nyumba ni muhimu sana kama ilivyo chakula, kwa Dar es Salaam kuna miradi ambayo tutaifanya sisi wenyewe na mingine kupitia sekta binafsi kwa maana ya Public-private partnerships (PPPs)
Amesema, hatua hiyo ina lengo la kuharakisha uendelezaji wa maeneo yaliyo wazi katikati ya miji kwa kujenga nyumba za vitega uchumi na hivyo kuliongezea shirika na nchi mapato makubwa.
Bw.Mchechu amesema kuwa, ujenzi huo utakwenda kujibu matatizo ya maeneo ya biashara na matatizo ya nyumba za makazi katikati ya miji.
"Tutajikita zaidi kwenye ujenzi wa maghorofa ambayo ni ya bei nafuu, na Watanzania wataweza kuyaishi na kuyanunua na taratibu maalumu ambazo zinasema watu waishije ni kama ambavyo ungeweza kukaa kwenye nyumba yako binafsi.
"Sisi tunajenga nyumba za kuuza, kupangisha na niseme tunajenga kwa watu wote hata tunapofanya maendelezo ya ubia kipaumbele kinaanza kwa yule ambaye anakaa kwenye ile sehemu, lakini siyo kwamba yeye ndiye mwenye haki pekee, kama anakuwa hajisikii basi huyo unamsaidia Mtanzania mwingine kwa sababu uhaba wa nyumba ni mkubwa kuliko unazoziona (zilizopo),"amesema Bw.Mchechu.
Awali, Bw.Mchechu aliwaeleza wawekezaji hao kuwa, katika mwaka huu wa fedha shirika linatarajia kutumia shilingi bilioni 413.7 kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema, mradi huo wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na wanatamani Watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo.
Bw.Mchechu amesema,asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa jijini Dar esSalaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine asilimia 30.
Pia amesema, nyumba hizo zitaanza kujengwa mwezi Septemba eneo la Kawe Dar es Salaam (nyumba 500) na Medeli jijini Dodoma (nyumba 100).
Aidha, amesema shirika linadhamiria kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Morocco Square ambao ujenzi upo kwenye hatua ya uboreshaji wa mandhari ikiwemo kukamilisha miradi ya Kawe 711 na Golden Premier Residence (GPR) iliyopo Kawe.
Katika hatua nyingine, Bw.Mchechu alitumia nafasi hiyo kuupongeza Ubalozi wa Afrika Kusini hapa Tanzania kwa kuendelea kuwashirikisha fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania wawekezaji kutoka nchini humo.
Naye Kaimu Balozi wa Afrika Kusini hapa Tanzania,Stella Vuyelwa Dhlomo-Imieka amesema kuwa,licha ya Tanzania na Afrika Kusini kuwa na uhusiano mwema na ushirikiano wa muda mrefu, wataendelea kuitumia diplomasia ya uchumi ili kuhakikisha wanawakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeza Tanzania.
Amesema kuwa, ushirikiano wa kiuchumi ni chachu kubwa ya kuyafikia malengo ya kuimarisha na kuharakisha maendeleo, na sekta ya nyumba ni miongoni mwa maeneo muhimu ambayo wanaamini uwekezaji ukifanyika vya kutosha licha ya kuweka mandhari ya kuvutia katika miji pia utawezesha wananchi kupata makazi bora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini, Bw.Manish Thakrar amesema, wanaamini Tanzania ni sehemu nzuri ya uwekezaji kutokana na sera na fursa nyingi za uwekezaji.
Amesema, wafanyabiashara wa Afrika Kusini wanaitazama Sekta ya Nyumba kwa ukubwa na wanaamini uwekezaji wao katika eneo hilo unaweza kuleta matokeo bora zaidi hapa nchini.