NA DIRAMAKINI
MELI ya Kimarekani ya Wanamaji iitwayo USS Hershel “Woody” Williams imewasili katika ziara ya bandari ya Dar es Salaam, Agosti 13, 2022.

“Tanzania ni mshirika muhimu wa Marekani katika kukuza amani na utulivu wa kikanda Afrika Mashariki nzima,” alisema Kept. Chad Graham, Afisa Mkuu wa Hershel “Woody” Williams. “Tunaishukuru sana Tanzania kwa kuturuhusu kufanya ziara hii ya bandari wakati tukiendelea na shughuli katika pwani nyingine.”
Hii ni ziara ya kwanza ya meli ya Kimarekani katika bandari baada ya zaidi ya muongo mmoja. Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright alisema ziara ya USS Hershel “Woody” Williams inaonyesha uimara wa ushirikiano wa kiulinzi kati ya Marekani na Tanzania.

Tanzania ni mshirika muhimu katika kudumisha amani na utulivu Magharibi mwa Bahari ya Hindi. Aidha, Tanzania ilishiriki katika zoezi la Cutlass Express, Februari 2022, zoezi la wanamaji linaloshirikisha mataifa mbalimbali lililofanyika Afrika Mashariki na Magharibi mwa Bahari ya Hindi. Aina hii ya mazoezi huimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi na kufanya kazi kwa karibu zaidi katika changamoto za pamoja za kimataifa.

Marekani ina maslahi ya pamoja na mataifa ya Afrika katika kuhakikisha ulinzi, usalama na uhuru wa safari katika maji yanayolizunguka bara, kwa sababu maji haya ni muhimu kwa ustawi wa Afrika na kuyafikia masoko ya dunia.