NA DIRAMAKINI
MUFTI Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubery amewasihi Watanzania wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa ambao sasa wanaendelea na zoezi la kuhesabu watu na makazi lililoanza tangu Agosti 23, 2022.
Sheikh Zubeir ametoa kauli hiyo nyumbani kwake jijini Dar es salaam, ambapo amesema yeye binafsi na familia yake tayari wameshahesabiwa ambapo ametumia nafasi hiyo kupongeza aina ya maswali yanayoulizwa na Makarani wa Sensa.
"Mimi nimeshamaliza zoezi la kuhesabiwa tena nimehesabiwa mimi na familia yangu yote na uzuri hakukua na maswali magumu yalikua maswali mepesi mepesi ambayo kila Mtanzania anayamudu kuyajibu" Amesema Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubeir
Aidha, Mufti Zubeir amewataka Watanzania ambao bado hawahesabiwa kwenye kuendelea kuwa watulivu kwani zoezi hilo litachukua kwa takribani siku saba hivyo Makarani watapita kwenye Kaya zao.
"Niwaambie Watanzania zoezi hili la kuhesabiwa halikua kwa siku moja tu ya Agosti 23, 2022 bali ni la siku saba kama bado hujahesabiwa basi tambua tu Karani atapita kwenye kaya na atakuhesabu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu,"ameongeza Mufti Zubeir.
Agosti 23, 2022 Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliongoza
kwa mfano kushiriki zoezi la Sensa kwa kutoa taarifa sahihi kwa Karani
wa Sensa aliyekwenda kumuhesabu.