Musoma Vijijini wazidi kutabasamu, wamshukuru Rais Samia

NA FRESHA KINASA

KATIKA kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea na kasi siku hadi siku ya usambazaji wa huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mheshimiwa Prof.Sospeter Muhongo leo Agosti 10, 2022 ikibainisha hayo na kutoa shukurani nyingi za kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kumtua mama ndoo kichwani kwa kusogeza karibu na wananchi huduma ya maji safi na salama ndani ya Jimbo hilo.

"Kasi ya kusambaza maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria inaongezeka siku hadi siku ndani ya Jimbo letu. Asante sana Serikali yetu chini ya uongozi mzuri sana wa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, vijiji vya kata ya Nyambono na Kata ya Bugoji vimeanza kupata maji kutoka Ziwa Victoria ikiwemo Kijiji cha Nyambono na Kijiji cha Saragana. Huku maji hayo ya bomba pia yatapelekwa hadi Kijiji cha Mikuyu Kata ya Nyamrandirira.

Aidha, vijiji hivi vimejengewa tenki la ujazo wa lita 200,000. Mlimani Nyabherango katika bajeti ya mwaka 2021/ 2022.
Upande wa Kata ya Bugoji ni pamoja na Kijiji cha Bugoji, Kijiji cha Kanderema na Kijiji cha Kaburabura ambapo takribani wakazi 12,000 wa vijiji hivyo wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama.

Na pia vijiji hivi vimejengewa tenki la lita 200,000 mlimani Nyabherango huku fedha za mradi huo zikiwa ni EP4R shilingi milioni 480 na fedha za UVIKO-19 shilingi milioni 500.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ndani ya Jimbo hilo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi jimboni humo.

Witness Mjinja ni mkazi wa Kitongoji cha Nyaberango Kijiji cha Nyambono ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga mradi huo ambapo kwa sasa upatikanaji wa maji ni wa uhakika.

Huku akimpongeza pia Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo kwa usimamizi madhubuti na ufuatiliaji makini ambao umeleta neema ya maji safi na salama kwa wananchi na hivyo kuondoa usumbufu kwa kina mama kwani muda mwingi walitumia kutafuta maji na kushindwa kufanya kazi za uzalishaji mali.
"Tulikuwa tukiamka usiku na kuacha waume zetu wakiwa wamelala na kulazimka kutembea umbali mrefu kutafuta maji katika visima vya asili ambayo pia hayakuwa safi na salama.

"Lakini kwa sasa tunaishukuru Serikali na Mbunge wetu Prof.Muhongo kwa namna ambavyo ameendelea kuihimiza serikali na kufanya ufuatiliaji wa miradi ili wananchi tuondokane na changamoto mbalimbali ikiwemo huduma ya maji safi na salama na sasa tunanufaika,"amesema Sarah Majaba.

Mwesa Malima ni mkazi wa Kijiji cha Bugoji amesema kuwa, wakati wa kiangazi ndoa nyingi zilikuwa na changamoto kwani wanawake walilazimka kuamka saa nane za usiku na kurudi nyumbani saa mbili hadi saa tatu za asubuhi na hivyo kuathiri shughuli nyingine za maendeleo katika familia.

Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Musoma, Mhandisi Chacha Mwise amesema mradi huo wa Bugoji-Kanderema-Kaburabura umegharimu jumla ya shilingi milioni 980 ambapo fedha za UVIKO-19 ni shilingi milioni 500 na EP4R shilingi milioni 480.

Huku akimpongeza Rais Samia kutoa fedha hizo kutekeleza mradi huo kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mheshimiwa Prof. Sospeter Muhongo anaendelea kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi jimboni humo ambapo leo Agosti 10, 22 alikuwa kata za Ifulifu Vijiji vitatu na Nyakatende Vijiji 4 ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu thabiti wajitokeze kuhesabiwa Agosti 23, mwaka huu ambayo ni siku ya Sensa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news