NGOs 39 kufutwa mkoani Mtwara

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI mkoani Mtwara inakusudia kuyafuta Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali 39 kutokana na kutokidhi matakwa ya kisheria ikiwemo kutohakiki taarifa zao na kutofanya kazi kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Lucy Mtepe akiwasilisha taarifa ya hali ya Mashirika hayo mkoani hapo mbele ya Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju Agosti 6, 2022.

“Kwa sasa mkoa una Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 51 yanayotoa huduma katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, elimu, huduma kwa makundi maalum na watoto waishio katika mazingira magumu. Katika uhakiki uliofanyika, Mkoa ulihakiki mashirika 66,mashirika yanayokusudiwa kufutwa ni 39,”amesema Mtepe.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Mpanju akifungua kikao hicho ameyataka Mashirika kutekeleza wajibu wa kufuata sheria na miongozo ya uendeshaji wake.

Mpanju pia ameyataka Mashirika hayo kushiriki katika kufanikisha Mkutano mkuu wa mwaka wa Mashirika hayo unaotarajiwa kufanyika Septemba 29, mwaka huu wenye lengo la kukutana wadau wote ili kujadili changamoto na kutambua mchango wa NGOs katika Jamii.

Ameongeza kwamba katika jukwaa hilo mwaka huu, mwongozo wa uendelevu wa mashirika hayo ya yasiyokuwa ya kiserikali utazinduliwa rasmi ili kupunguza utegemezi wa wafadhili.

“Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mmekuwa na mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Taifa letu, nyie ni mkono wa kuume wa Serikali kwa misingi ya kuwafikia wananchi mahali Serikali haiwezi kufika” amesema Mpanju.

Kwa upande wake Katibu Tawala mkoa wa Mtwara Abdallah Malela amesema changamoto ni taasisi kukosa muendelezo kwa kutegemea ufadhili kwa kadri siku zinavyokwenda ufadhili unapungua hivyo wanatakiwa wabuni shughuli za kuongeza kipato.

Naye Mmoja wa mwakilishi wa NGOs Mustapha Mwiyunga ameishukuru Serikali kwa kuliona suala la uendelevu wa Mashirika bila kutegemea wafadhili na kulitafutia suluhisho.

“Tunashukuru na tunaomba tupate dondoo za mwongozo huo ili tujiandae mapema ni namna gani tunajipanga kwa uendelevu” amesema Mwiyunga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news