NHIF kuja na maboresho makubwa zaidi nchini

*Lengo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma

NA MWANDISHI WETU

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), unatarajia kufanya maboresho mbalimbali kwenye huduma inazozitoa kwa lengo la uimarishaji na upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama wake.
Akiwasilisha mada kwenye mkutano wa wadau wa Mfuko ambao ni Watoa Huduma, Wanachama na Waajiri uliofanyika jana Mkoa wa Singida, Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama Bw. Christopher Mapunda alisema maboresho hayo yana nia ya kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa haraka na ubora zaidi.

Alielezea maboresho hayo yatauwezesha Mfuko kuwa na taarifa sahihi za wanufaika na mfumo madhubuti wa utambuzi wa wanachama, kuimarisha ubora wa upatikanaji wa huduma, kuondoa usumbufu na kukinga afya za wanufaika.

“Maboresho haya pia yanakwenda kuondoa malalamiko kutoka kwa wadau kutokana na mapungufu katika kitita cha mafao kinachotumika hivi sasa kwa kuwa tunakwenda kuhuisha Kitita cha Mafao kwa kuzingatia Mwongozo wa Tiba nchini (STG), Orodha ya Dawa Muhimu ya Taifa (NEMLIT), Sheria ya Mfuko na Mapendekezo ya Taarifa ya Tathmini ya Uhai na Uendelevu wa Mfuko na kuboresha Kanuni za Mfuko,” alisema Bw. Mapunda.
Katika uimarishaji wa mifumo Bw. Mapunda alisema kuwa, Mfuko utaunganisha mifumo na taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Mamlaka ya Mapato (TRA), Wakala wa Usajli wa Kampuni (BRELA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ili kuwezesha utambuzi wa wanachama wachangiaji itakayosaidia kuondoa malalamiko na usumbufu unaojitokeza hasa nyaraka zinapoonekana kuwa na changamoto.

“Mfuko utaweka utaratibu wa uchangiaji kwa awamu kabla ya kuanza kupata huduma lengo ni kuweka unafuu katika uchangiaji kwa wananchi ili wajiunge na bima ya afya, kuwezesha kuwasilisha taarifa ikiwemo michango kwa njia ya kieletroniki kwa kuimarisha portal ya waajiri na kuendelea kuwezesha wanachama kupata taarifa muhimu kupitia simu zao za mkononi,” alisema Bw. Mapunda.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Bw. Juma Muhimbi aliwataka wadau wake wote kuulinda uhai wa Mfuko kwa wivu mkubwa kwa kutoa taarifa za udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watoa huduma, wanachama na wananchi wengine wasio waaminifu.

“Ndugu zangu mtakubaliana na mimi kuwa tunauhitaji huu Mfuko ili utuhudumie lakini kumekuwepo na wimbi kubwa la udanganyifu, niwaombe sana kila mmoja awe mlinzi wa huduma zinazotolewa na Mfuko ili uzidi kuwa imara zaidi,” alisema Bw. Muhimbi.

Akizungumzia Watoa Huduma amewataka waendelee kutoa huduma bora kwa wanachama na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu ili kuwezesha Mfuko kulipa madai halali lakini pia kuwa mabalozi wa kutoa taarifa sahihi na sio kuelekeza lawama kwa Mfuko pale inapoonekana huduma fulani haipo.

“Wanachama niwaombe sana kila mmoja ahakikishe kadi yake matibabu haitumiki na mtu mwingine kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kuhujumu Mfuko huu lakini pia kwa Waajiri wahakikishe wanawasilisha michango ya Watumishi wao kwa wakati ili kuepukana na usumbufu kwa wafanyakazi na wategemezi wao kukosa huduma kutokana na kukosekana kwa michango,” alisisitiza Bw. Muhimbi.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Bw. Bernard Konga, aliwahakikishia wanachama kuwa, uhai wa Mfuko uko imara na unaendelea kuwahudumia wanachama wake kwa huduma wanazozihitaji.

“Mfuko uko imara sana na kwa sasa tunajivunia sana uimarishaji wa huduma ambao umefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Hassan Suluhu hususan kwa kuweka vifaa tiba vya kisasa katika hospitali mbalimbali nchini ambayo inarahisisha zaidi upatikanaji wa huduma kwa wanachama wetu hivyo kama Mfuko tunaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi ili wajiunge na Mfuko,” alisema Bw. Konga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news