OR-TAMISEMI yapokea maelekezo ya USEMI kuhusu barabara ya Kidabaga-Bomang'ombe

NA OR-TAMISEMI

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imesema imepokea maelekezo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa (USEMI) ya kukamilisha kipande cha kilomita moja cha barabara katika Barabara ya Kidabaga-Bomang'ombe iliyopo wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Ni bada ya USEMI ikiongozwa na mwenyekiti wake, Mheshimiwa Abdallah Ulega kutembelea barabara hiyo ya Kidabaga hadi Bomang'ombe yenye urefu wa kilomita 18.3 iliyojengwa kupitia mradi wa “Agri-Connect.

Akizungumza katika ziara hiyo,Naibu OR-TAMISEMI (Afya), Mheshimiwa Festo Dugange alisema kuwa, ofisi yake imepokea maelekezo yote ya kamati na kuahidi kuyatekeleza kwa kuanza na ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita moja ifikapo Oktoba 30, mwaka huu.
Pia Mheshimiwa Dugange amesema,wizara imechukua maelekezo ya kamati ya kujenga barabara zote za lami kwa kuanzia uzito wa tani 30 na kuendelea ili wananchi wasafirishe mazao yao vizuri, na kuahidi kutekeleza maaagizo hayo.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya USEMI, Mhe. Abdallah Chaurembo (Mb), aliiagiza TARURA kukamilisha kipande cha kilomita moja kilichobaki pamoja na kuhakikisha kuwa barabara zote zitakazojengwa na TARURA zijengwe kwa kuhimili uzito wa tani 30, ili wananchi wanufaike kwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kwa urahisi.

Wakati huo huo, wananchi wa Kata ya Bomang'ombe wilayani Kilolo wameelezwa kufurahishwa na ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa (USEMI), iliyotembelea wilayani humo kukagua barabara hiyo.

Akiongea kwa niaba ya wananchi wa Boman'gombe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bomang'ombe, Elia Boing'ombe alisema kuwa, ujio wa kamati hiyo ni faraja kubwa sana kwao kwa sababu wanaamini ujio wao ni uwepo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mwenyewe hivyo shida zao zote zitatuliwa.
“Kwa kweli tunaona ni muujiza kwa kamati hii kufika hapa sababu hatujawahi kupata ugeni kutoka bungeni. Napenda kuwashukuru kwa sababu pamoja na Mheshimiwa Rais, tayari mmeshatupendelea kipande hiki cha kutoka Kidabaga hadi Bomang'ombe kwa kiwango cha lami, sasa tunaamini ujio wenu utamaliza na hii kilomita moja iliyobaki,”alisema Boing'ombe.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilolo, Mhe.Justin Nyamoga ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo alisema kuwa, eneo la Bomang'ombe ni maarufu sana kwa kilimo cha mazao ya mbogamboga hivyo ujio wa barabara hiyo ni faraja kubwa kwao.

“Kutokana na changamoto ya barabara iliyokuwepo haya mazao wakati mwingine yalikuwa yanachukua hadi wiki moja kufika Kidabaga, lakini tunamshukuru Mheshimwa Rais kwa sababu sasa tunapita bila shida na mazao yanafika haraka Kidabaga na ndiyo maana tunalilia kile kipande cha kutoka Kidabaga kwenda Kilolo nacho kimaliziwe tuunganishe mpaka mwisho,“alisema Nyamoga.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya USEMI imemaliza ziara yake ya siku nne mkoani Iringa baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za lami za mradi wa Agri-Connect unaotekelezwa chini ya ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya.

Mradi huu unalenga kuwasaidia wakulima vijijini kuimarisha mnyororo wa thamani ya mazao yao hasa mazao ya chai, kahawa, mbogamboga na mazao mengine yanayohitaji kusafirishwa kwa haraka toka mashambani hadi viwandani na sokoni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news