PIGA SIMU HESABIWA: Popote pale sikia, ni haki yako kuhesabiwa

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

AGOSTI 29, 2022 Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022,Mheshimiwa Anne Makinda amesema asilimia 93.45 ya kaya zote Tanzania zilikuwa zimehesabiwa hadi kufikia asubuhi ya saa 2.
Mheshimiwa Makinda amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya Sensa ya Watu na Makazi ambapo ilianza Jumanne ya Agosti 23, 2022.

Kwa mujibu wa Kamisaa, haya ni mafanikio makubwa yaliyotokana na utayari mkubwa wa wananchi kushiriki kuhesabiwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Amesema taarifa zilizokwishakusanywa zinaonesha bado kuna asilimia 6.55 ya kaya ambazo hazijahesabiwa.

Makinda ametoa muongozo kwa wananchi ambao watakuwa hawajahesabiwa mpaka kufikia jana jioni kuwa bado wana nafasi ya kuhesabiwa akitoa utaratibu ikiwemo kwenda kwenye ofisi za serikali za mitaa wanakoishi.

Mwananchi unashauriwa uende moja kwa moja kwenye ofisi za Serikali za mitaa na onana na mwenyekiti au mtendaji wa mtaa unaoishi na hakikisha unawachia namba ya mawasiliano ili karani akufuate ulipo na kuanza kazi ya kukuhesabu.

Kutokana na umuhimu wa kipekee wa sensa, mshairi wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anakushirikisha jambo muhimu ambalo litakuwezesha ambaye bado haujahesabiwa uweze kuchangamkia fursa kwa manufaa yako na Taifa kwa jumla, karibu;

1. Ni bora utupigie, upate kuhesabiwa,
Na wala usisinzie, ukose kuhesabiwa,
Namba uziangalie, piga upate fikiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

2. Zoezi linaishia, hakiki wahesabiwa,
Tunakuhakikishia, na wewe utafikiwa,
Popote pale sikia, ni haki kuhesabiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

3. Tumefikia pazuri, ni wengi wamefikiwa,
Lakini tuna hadhari, pengine hujafikiwa,
Usikae kusubiri, ita utahesabiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

4. Heko kwa Watanzania, nyote mliofikiwa,
Na wageni wenye nia, mlokwishahesabiwa,
Nyie mliosalia, tafadhali hesabiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

5. Muhimu ukafikiwa, wala usijechelewa,
Umuhimu waelewa, takwimu zinawaniwa,
Mipango tukipangiwa, iwe tunayoelewa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

6. Tuko mwishoni mwishoni, muhimu kuhesabiwa,
Wala usione soni, piga simu hesabiwa,
Wako wengi makarani, hakika utafikiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

7. Tupo tayari tayari, simuyo yasubiriwa,
Ukipiga ni habari, karani utatumiwa,
Takuhesabu vizuri, nasi tutafurahiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

8. Mmesalia wachache, ni bado kuhesabiwa,
Tokeza usijifiche, takwimu zinawaniwa,
Kupiga simu siache, na wewe utafikiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

9. Asanteni ninyi nyote, mlokwishahesabiwa,
Shukurani mzipate, kweli tumewaelewa,
Kesho takwimu tupate, vema zipate tumiwa,
Sensa kwa ajili yetu, usikose hesabiwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news