RAIS ATUKUMBUSHA:Manufaa tutapata,kwa huduma kupatiwa, Sensa ni taarifa sahihi

NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)

MTAKWIMU Mkuu wa Serikali nchini, Dkt. Albina Chuwa amesema hadi kufikia Agosti 25, 2022, kaya milioni tano zimeshahesabiwa nchi nzima sawa na idadi ya watu milioni 22.
Kati ya hao wanawake ni milioni 11.4 sawa na asilimia 51.9 na wanaume ni milioni 10.5 sawa na asilimia 48.1.

Dkt.Chuwa amebainisha kuwa, uchambuzi unaonesha mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweza kuhesabu watu kwa wastani wa asilimia 36.8. Mkoa unaoongoza kwa kasi kubwa ni Kaskazini Unguja ambapo asilimia 49.7 ya kaya zote zimeshahesabiwa.

Mtakwimu huyo amesema hayo katika kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu Sensa ya Watu na Makazi iliyoanza Agosti 23, 2022.

Haya ni mafanikio makubwa,ikizingatiwa zoezi hilo litafikia tamati Agosti 30, mwaka huu, hivyo bado mwitikio wa Watanzania kushiriki kwa kutoa taarifa zote muhimu na kwa usahihi kwa makarani ni muhimu, kwa kulitambua hilo, msahiri wa kisasa, Bw.Lwaga Mwambande anakushirikisha jambo lifuatalo kupitia shairi, karibu;

1.Rais atukumbusha, tuweze kuhesabiwa,
Ujumbe metuamsha, tusije tukachelewa,
Sensa ni kuhakikisha, kwamba sote twafikiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

2.Agosti shina tatu, lianza kuhesabiwa,
Weshahesabiwa watu, ambao wamefikiwa,
Tena bado wengi watu, wanazidi hesabiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

3.Wiki nzima ni zoezi, la watu kuhesabiwa,
Kusiwepo kizuizi, cha kutokuhesabiwa,
Hata ukiwa na kazi, kumbuka kuhesabiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

4.Agosti shina nne, wengi wamehesabiwa,
Na hata siku zingine, twazidi kuhesabiwa,
Lengo wala si jingine, litakalo kufikiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

5.Ya kwamba siku ya kwanza, wengi walihesabiwa,
Vema sensa tulianza, vile watu waelewa,
Mbele tusijejiponza, kwa tusiohesabiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.


6.Takwimu tukizipata, baada kuhesabiwa,
Mipango tutayopata, Serikali kupangiwa,
Manufaa tutapata, kwa huduma kupatiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

7.Takwimu sawa chakula, kile kinapakuliwa,
Idadi ya wanaokula, muhimu kuielewa,
Isijefika pahala, wengine kutofikiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

8.Endapo tuko sitini, milioni twaelewa,
Huduma za milioni, ishirini kutolewa,
Vigumu kuona ndani, wote kuweza fikiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

9.Ni umuhimu wa sensa, sote tukihesabiwa,
Utatibu hilo hasa, tuweze kufanikiwa,
Ndiyo maana twaasa, muhimu kuhesabiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

10.Mahitaji maalumu, yale yanahitajiwa,
Wale wale maalumu, ili waweze patiwa,
Idadi yao muhimu, mipango wakapingiwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

11.Simu unayetumia, ujumbe mesambaziwa,
Ukishasoma sikia, hakiki mehesabiwa,
Kote watakufikia, sije kusahauliwa,
Ni taarifa sahihi, ndizo zinahitajika.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news