NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha inasaidia upatikanaji wa usafiri pamoja na vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya Jeshi la Polisi Zanzibar ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Dkt. Mwinyi amesema hayo Agosti 4, 2022 Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na Kamishna mpya wa Polisi Zanzibar, CP Hamad Khamis Hamad, aliyefika kujitambulisha.
Amesema, pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na dhima ya moja kwa moja kushughulikia masuala ya usafiri na mawasiliano kwa Jeshi la Polisi Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaifanyia kazi changamoto ya upungufu wa magari pamoja na vifaa vya mawasiliano inayolikabili jeshi hilo ili liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na uongozi wa jeshi hilo, huku akimpongeza Kamishna huyo kwa uteuzi huo.
Aidha, amempongeza Kamishna Hamad kwa kukabidhiwa jukumu hilo, ikizingatiwa uzoefu wa kutosha alionao pamoja na na kuifahamu vyema Zanzibar katika masuala mbalimbali, yakiwemo ya kiuhalifu.
Naye Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad alimuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Mwinyi kuangalia uwezekano wa kusaidia upatikanaji wa usafiri pamoja na vifaa vya mawasiliano pale hali itakaporuhusu, ili kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza vyema majukumu yake ya kukabiliana na uhalifu.
Amesema Jeshi la Polisi Zanzibar, kama ilivyo kwa Jeshi la Polisi Tanzania, linakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya usafiri na upungufu wa vifaa, hususan vya mawasiliano.
Pia amesema, upatikianaji wa vifaa hivyo ni muhimu katika kukabiliana na makosa mbali mbali, akibainisha huwazesha askari kufika maeneo ya matukio wa wakati muafaka.
Amesema, katika kipindi hiki Uongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar unaendelea kushughulikia mradi wa Ujenzi wa majengo mbali mbali, ikiwemo nyumba za Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja, kituo cha Polisi Mkokotoni pamoja na ukarabati wa majengo ya Polisi Ziwani Unguja.
Aidha, CP Hamad alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri hya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kwa uteuzi wake na kubainisha faraja kubwa aliyonayo kutokana uteuzi huo, huku akisiistiza azma yake ya kushirikiana kikamilifu na taasisi na Vikosi vya SMZ katika kukabiliana na uhalifu nchini.