NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo yatakayopata misaada kutoka jumuiya hiyo kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt.Mwinyi ametoa shukrani hizo alipozungumza na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga aliyefika Ikulu jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na mazungumzo mafupi.
Amesema, ni jambo jema kwa Zanzibar, hususani Kisiwa cha Pemba kuwa miongoni mwa maeneo ambapo miradi mbalimbali ya maendeleo itatekelezwa chini ya ufadhili wa EU hapa Tanzania, ikiwemo Mradi wa Kuboresha Mtazamo wa Majiji (Green City), ambao unakusudiwa kutekelezwa katika miji mitatu ya Tanzania ya Tanga, Mwanza na Pemba.
Amesema, tangu Serikali ya Awamu ya Nane iingie madarakani ikiwa na mfumo wa Umoja wa Kitaifa (GNU), kumekuwepo dalili za EU kurejesha uhusiano wake na Zanzibar kufuatia kuwepo kwa demokrasia.
Aidha, Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa,utalii ni sekta kuu ya Uchumi wa Zanzibar, na kusema Zanzibar imejipanga kuimarisha sekta hiyo baada ya kuathirika kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19.
Alimtaka Balozi huyo kuendeleza mazungumzo na mamlaka zinazosimamia utalii nchini Ubelgiji ili kufanikisha lengo la kuwepo safari za ndege za moja kutoka Ubelgiji hadi Zanzibar na hivyo kuleta matumaini ya kuongeza ujio wa watalii hapa nchini.
Akigusia suala la kuwepo fursa za biashara nchini Ubelgiji, Dkt.Mwinyi amesema, Diplomasia ya Uchumi inazingatia umuhimu wa kuangalia fursa za biashara, hivyo akasema pamoja na kuwepo changamoto mbalimbali katika utayarishaji wa dagaa kwa wajasiriamali hapa nchini, Serikali itaishughulikia changamoto hiyo hatimae fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo.
Pia amesema, Zanzibar imekuwa ikishughulikia miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo, hivyo kuwepo kwa taasisi zinazotoa mikopo nafuu ni jambo jema na kubainisha namna Serikali itazingatia namna itakavyoweza kupata mikopo hiyo kupitia mashirika hayo ya fedha yaliopo EU.
Aidha, alisema Zanzibar itashukuru kupata fedha za mkopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kupitia Sekta ya Uchumi wa Buluu.
Mapema Balozi wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania nchini Ubelgiji ambapo pia anaiwakilisha Tanzania nchini Luxenbourg na Jumuiya Umoja wa Ulaya (EU), Jestas Nyamanga amesema kuanza kwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya Ubelgiji na Zanzibar kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu, kutaongeza idadi ya watalii watakaozuru nchini.
Amesema, mawasiliano yamefanyika kuona kunakuwepo usafiri wa ndege ya moja kwa moja kati ya Ubelgiji -Zanzibar kwa wastani wa mara mbili kwa wiki na hivyo kuongeza idadi ya ujio wa watalii baada ya kuathirika kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19, ambapo kabla ya ugonjwa huo wastani wa watalii 16,000 walikuwa wakizuru nchini kila mwaka.
Amesema katika mazingira ya sasa watalii kutoka nchi hiyo hutumia Shirika la Ndege la Qatar, jambo ambalo lina changamoto mbalimbali.
Aidha, alisema nchi hiyo ina fursa mbalimbali za msomo ya juu, hususan katika kiwango cha Master na PHD, hivyo akatoa wito kwa Vyuo vikuu vya Zanzibar, ikiwemo SUZA pamoja na wananchi wengine wenye uwezo kuhamasika ili kutumia fursa zilizopo.
Balozi Nyamanga alisema, mahusiano kati ya Tanzania na Ubelgiji yameimarika na kubainisha fursa kadhaa za kibiashara, ambapo Tanzania inaweza kufanya, ikiwemo kuuza minofu ya samaki, dagaa, mbogamboga, mchele pamoja na viungo vya aina mbalimbali.
Amesema, Zanzibar inaweza kunufaika na fursa hiyo kupitia uuzaji wa dagaa, mkazo ukiwekwa katika utayarishaji na uhifadhi bora wa dagaa hilo ili kuliongezea thamani, pamoja na usafirishaji wa viungo ikiwemo pilipili.
Kuhusiana na uwekezaji, Balozi Nyamanga alisema Luxembourg ni kituo kikuu cha Mashirika ya Fedha pamoja na Mabenki huku akibainisha kuwepo kampuni zinazoonesha nia ya kutoa mikopo nafuu kwa Zanzibar, hivyo akaiomba Serikali kubainisha maeneo yanayoweza kutumika.
Akizungumzia mahusiano ya Tanzania na Jumuiya Umoja wa Ulaya, Balozi Nyamanga alisema kuwa ni mazuri, ambapo EU imekuwa ikiendelea kutoa misaada hususani ya kifedha kwa Tanzania.
Alisema, EU imetenga kiasi cha Euro milioni 554 kwa Tanzania ili kuiwezesha kuingia katika soko la Ulaya pamoja na Euro milioni kumi kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa asali ya nyuki.
Aliitaja mikoa ya Katavi, Rukwa, Tabora, Dodoma, kisiwani Pemba kuwa itanufaika na msaada huo, lengo likiwa ni kuzalisha asali yenye viwango.
Aidha, alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2021-2027 EU imeahidi kusaidia Tanzania kiasi cha Euro milioni 425, ambapo Euro milioni 703 zimelengwa katika uboreshaji wa mitazamo ya majiji (green city) katika miji mitatu ya Tanga, Mwanza pamoja na Pemba.
Alisema, fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuimarisha miundombinu pamoja na masoko katika miji hiyo.
Aidha, Balozi huyo aliishukuru Serikali kwa kutilia mkazo uimarishaji wa sekta ya Uchumi wa Buluu akibainisha kiasi cha Euro milioni 140 zilizotengwa na jumuiya hiyo kwa ajili ya uimarishaji wa Uchumi wa Buluu ambapo miongoni mwa matumizi yake yatahusisha mikopo kupitia sekta binafsi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Balozi wa Shirikisho la Kidemokrasia Jamhuri ya Ethiopia nchini Tanzania, Mhe. Shibru Mamo Kedida, alipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo.(Picha na Ikulu).
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alikuwa na mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania, Shibu Mamo Kedida.
Katika mazungumzo hayo yaliofanyika Ikulu jijini Zanzibar viongozi hao walizungumzia haja ya kuendeleeza mahusiano na mashirikiano ya kihistoria kati ya Zanzibar na Ethiopia katika njanja mbalimbali kwa maslahi ya mataifa hayo na wananchi wake.
Miongoni mwa maeneo ya mashirikiano yaliogusiwa ni pamoja na utalii,michezo,utamaduni,masuala ya anga pamoja na elimu.