Rais Dkt.Mwinyi aomboleza kifo cha Mwenyekiti wa TLP, Augustine Lyatonga Mrema

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameelezea kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustine Lyatonga Mrema.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyaeleza hayo leo Agosti 21, 2022 huku akibainisha kuwa, Mrema atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa taifa dhidi ya wala rushwa.
"Nimesikitishwa na kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Bw. Augustine Lyatonga Mrema kilichotokea leo asubuhi Dar es Salaam.

"Ikumbukwe Bw.Mrema alitoa mchango mkubwa kwa taifa katika mapambano dhidi ya wala rushwa. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, Amin,"ameeleza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Awali, Mrema ambaye alizaliwa Desemba 31, 1944, Vunjo mkoani Kilimanjaro kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Buberwa Aligaesha alilazwa hospitalini hapo kuanzia Agosti 16,2022 na kufikwa na mauti asubuhi ya leo Agosti 21,2022 saa 12:15.

Mrema aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77.

Enzi za uhai wake, Mrema aliwahi kuwa mgombea urais kupitia NCCR-Mageuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, akichuana na Hayati Benjamin Mkapa baada ya kujiunga na chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mrema aliwahi kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Temeke (NCCR Mageuzi) na Vunjo kupitia TLP na hadi amefikwa na mauti alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole nchini Tanzania.

Parole ni nini?

Bodi ya Taifa Parole ni tasnia muhimu sana katika urekebishaji wa wahalifu kwa kuishirikisha jamii. Tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo mwaka 1994, mafanikio makubwa yameonekana kutokana na baadhi ya wafungwa kuachiliwa kupitia utaratibu huo, hivyo kupunguza sehemu ya changamoto ya msongamano magerezani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news