Rais Dkt.Mwinyi atoa wito kwa wakulima na wafugaji

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewahimiza wakulima na wafugaji wanaoshiriki Maonesho ya Nanenane kuitumia vyema fursa hiyo kutafuta elimu ya matumizi sahihi ya zana za kisasa, mbegu bora na pembejeo ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuleta Mapinduzi ya Kilimo na Ufugaji nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Husein Ali Mwinyi akimsikiliza Waziri wa Uchumi wa Buluu Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame, wakati alipotembelea banda la wizara hiyo, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Kizimbani Wilaya ya Magharibi “A” Unguja na kushoto kwa Rais ni mkewe,Mama Mariam Mwinyi na kulia kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi ametoa wito huo katika Ufunguzi wa Maonesho ya Kilimo Nanenane yaliyofanyika Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema, wakulima na wafugaji wanapaswa kuyatumia maonesho hayo katika kutafuta elimu inayohusu matumizi ya zana za kisasa, upatikanaji wa mbegu bora, elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na njia za kupambana na maradhi yanayoathiri sekta hizo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, kuwepo kwa maonesho hayo kunatoa fursa kwa wananchi kuona mbinu za kisasa za kilimo, ufugaji, uvuvi pamoja na shughuli mbalimbali za kibiashara na ujasiriamali.
Pia amesema, maonesho hayo yanatoa fursa ya kuwakutanisha ana kwa ana wadau mbalimbali, wakiwemo wazalishaji na wateja wao, hatua inayotoa mchango mkubwa katika kukuza na kuongeza ubunifu, kutambua mafanikio, changamoto pamoja na upatikanaji wa masoko.

Akigusia kauli mbiu ya maonesho hayo isemayo ‘Kilimo ni Biashara, Shiriki kuhesabiwa kwa Mipango bora ya Sekta ya Kilimo’,Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, kaulimbiu hiyo imekuja kwa wakati mwafaka kwa kuzingatia changamoto kadhaa zinazoikabili Dunia na kutishia kuathiri hali ya Usalama wa Chakula.

Amesema, sekta zote za uzalishaji na usafirishaji zimeathirika kutokana na janga la UVIKO-19 pamoja na mgogoro ulioibuka baina ya mataifa ya Urusi na Ukrane ambayo ni mataifa yenye mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula,hususani ngano pamoja na uzalishaji wa mbolea na pembejeo.
Amesema, athari hizo zimeifanya Serikali kupunguza ushuru na kufidia bei za bidhaa muhimu na hivyo kuathiri kiwango cha ukusanyaji mapato na kuongezeka kwa matumizi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema Wizara Kilimo, Umwagiliaji, Maliasi na Mifugo ina jukumu la kuwa na mikakati madhubuti itakayoliwezesha taifa kuongeza uzalishaji na kuondokana na utegemezi wa bidhaa za chakula kutoka nje.

Pia amesema, ni muhimu kuendeleeza kilimo cha kisasa kwa kuwashajiisha makundi ya vijana kujishughulisha na sekta ya kilimo ili kuiongeza mchango wake na kukuza ajira.

“Wito wangu tuendelee kuyaimarisha mfafanikio tuliyopata kwa kuwashajisha vijana wengi zaidi kushiriki katika sekta ya kilimo kwa kuwapatia vifaa vya kisasa, mbegu bora na taaluma juu ya matumizi bora na sahihi ya pembejeo,” amesema.
Aidha, Dkt.Mwinyi amewakumbusha wakulima na wananchi kuongeza uzalishaji wa bidhaa za matunda na bidhaa nyingine zitokanazo na uvuvi kwa kigezo cha kuwepo mahitaji makubwa hotelini, wakati huu bidhaa hizo zikiagizwa kutoka nje ya nchi.

Akizungumzia uzalishaji wa zao la mpunga, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza kilimo cha zao hilo kwa njia ya umwagiliaji maji, ambapo jumla ya hekta 1,053 zinaendelezwa katika mabonde mbalimbali Unguja na Pemba.

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakulima watakaopata vitalu katika mabonde hayo kuvitunza na kuviendeleza ili lengo la Serikali la kuendeleza miradi mikubwa ya umwagiliaji maji kuona inafanikiwa.

Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kushajiisha wawekezaji kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi, pamoja na kuzifanyia kazi changmoto ziliopo za upatikanaji wa mbegu bora, vifaranga pamoja na chakula cha mifugo.

Amesema, kazi hiyo inapaswa kwenda sambamba na juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kulima na kuhifadhi maliasili za misitu ikiwemo mikoko.

“Tushirikiane kuyalinda na kuyatumia vizuri maeneo yaliotengwa kwa shughuli za kilimo na kuendelea kuhimizana juu ya upandaji miti ya matunda na ile ya asili,”amesema.

Aidha, Dkt.Mwinyi alirudia kauli yake ya kusisitiza umuhimu wa kuendeleza kilimo cha mikarafuu ili kuongeza uzalishaji, akibainisha kuwa na umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Uchumi wa Zanzibar.
Aliupongeza uongozi wa Serikali Awamu ya Saba kwa kuja na mpango maalum wa miaka 10 wa kufufua zao hilo, na kutilia mkazo upandaji wa miche mipya, ushughulikiaji mashamba, kutoa mikopo pamoja na bima kwa wakulima.

Aliuagiza uongozi wa Wizara Kilimo, Umwagiliaji, Maliasi na Mifugo kushirikiana na Shirika la Biashara (ZSTC) , pamoja na viongozi wa mikoa na wilaya kuongeza kasi ya upandaji wa mikarafuu mipya, akibainisha kuwepo maeneo mengi katika kisiwa cha Unguja ambayo zao hilo hustawi na bado hayajatumika ipasavyo.

Katika hatua nyingine, Dkt.Mwinyi aliitaka wizara hiyo kuwa na mipango imara na endelevu ya kuzalisha miche ya miti ya matunda na miti ya asili na kuigawa bure kwa wakulima katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba.

Aidha, aliitaka wizara hiyo kuongeza kasi katika kufanya tafiti mbalimbali za kilimo na baadae kusambaza matokeo yake, sambamba na na kushajiisha matumizi ya tafiti hizo kwa wadau.

“Serikali imeanzisha Taasisi ya Kilimo na taasisi nyingine za mifugo ili zituwezeshe kuondokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo,”amesema.

Amebainisha kuwa, tafiti hizo zinahitajika ili kupata mbegu bora na kupambana na maradhi, pamoja na wadudu waharibifu wa matunda.

Naye Waziri wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis amemhakikishia Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi kuwa, maelekezo na miongozo inayotolewa itashughulikiwa na kusimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha kunakuwepo upatikanaji wa uhakika wa chakula hapa nchini.

Amesema maonesho hayo yameweza kufanikiwa kufanyika kutokana na mashirikiano makubwa kati ya wizara hiyo na wadau mbalimbali, bila kuwepo matumizii ya fedha za bajeti ya Serikali.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Seif Shaaban Mwinyi alisema maonesho hayo yamewashirikisha wajasiriamali 155 kutoka taasisi 52, ambapo jumla ya shilingi milioni 78 zimetumika hadi sasa, kutokana na michango na ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali.

Amesema azma ya wizara hiyo ni kulizungushia uzio eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 9.4 ili liweze kutumika kwa shughuli za maonesho muda wote.
Katika hafla hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi amepata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali na kuangalia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wakulima na wafugaji.

Aidha,viongozi mbalimbali wa Kitaifa walishiriki katika hafla hiyo, akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news