NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Sekta ya Mafuta na Gesi asilia ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amesema hayo leo Agosti 10, 2022 Ikulu jijini Zanzibar katika hafla ya Makabidhiano ya Data za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa Vitalu vya Zanzibar, kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kupitia Wizara ya Nishati na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.
Amesema, kuna kila dalili zinazoonesha kuwepo kwa mafuta na gesi asilia hapa nchini hususan katika kitalu cha Pemba-Zanzibar na kubainisha ukubwa wa jambo hilo Duniani katika ukuzaji wa uchumi pamoja na namna nchi itakavyoweza kubadilika pale mafuta hayo yatakapoanza kuchimbwa.

Dkt. Mwinyi amewataka wawekezaji wa sekta ya Mafuta na Gesi asilia kuja nchini ili kuendeleza kazi za utafutaji wa nishati hizo na hatimaye kuweza kuchimba.
Ametumia fursa hiyo kushukuru mashirikiano makubwa yaliopo kati ya taasisi zinazoshughulikia suala hilo, Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (PURA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), hususan katika suala la upatikanaji wa mafunzo kwa watendaji wa Mamlaka ya udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA).
Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa, ushirikiano uliofanyika ni moja ya maeneo yanayoimarisha zaidi Muungano wa Tanzania na kusema wakati umefika wa kumaliza changamoto chache za Muungano zilizosalia, huku akibainisha na suala hilo limekaaa sawa kisheria na kisiasa.

Aidha, Dkt. Mwinyi amezitaka taasisi zinazoshughulika na uandaaji wa miundombinu ya kuhifadhi Data za utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia Zanzibar kujenga miundombinu hiyo haraka inavyowezekana ili iweze kutumikwa kwa shughuli za uhifadhi.
Dkt. Mwinyi amewashukuru viongozi waanzilishi wa suala hilo, akiwemo Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (Awamu ya Saba), Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kazi kubwa na nzuri ya kuliwekea misingi jambo hilo.

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa hatua anazochukua kujenga uchumi wa Taifa kwa Serikali zote mbili kupitia sekta ya mafuta na Gesi asilia.
Naye, Waziri wa Nishati wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania January Makamba alisema shughuli za utafutaji wa mafuta zilizokusanywa zimeanzia miaka ya 1950 katika vitalu namba 9,10,11 na 12 pamoja na Kitalu cha Pemba- Zanzibar.
Amesema, tayari visima 96 vimeshachimbwa ambapo visima 44 vimegundulika kuwa na Gesi asilia kwa wastani Futi za Ujazo trilioni 57.4.

Alisema kuwepo kwa taarifa hizo kutawahamasisha na kuwavutia watafutaji wa Mafuta na gesi asilia , kwa kigezo kuwa itakuwa ni rahisi kwao kupata pa kuanzia.
Aidha, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Suleiman Masoud Makame alisema mapokezi hayo ya Data yamefanyika huku kukiwa na dhamira ya dhati ya serikali katika kufanikisha jambo hilo kwa vitendo na kutumia fursa hiyo kuwaahidi Wazanzibari kuwa litafanyika kwa umakini mkubwa.

Alisema Data hizo zitakuwa kichocheo kikubwa cha Uwekezaji katika sekta ya Mafuta na Gesi Asilia na kupongeza mashirkiano makubwa yalioonyeshwa kati ya taasisi zinazoshughulikia suala hilo, hususan katika suala la upatikanaji wa mafunzo na uhifadhi bora wa Data.
Alisema hatua hiyo inaakisi utekelezaji wa vitendo wa miongozo ya Viongozi, sheria pamoja na Katiba za Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya zanzibar.