NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imekubali siku ya Mwaka mpya wa Kiislamu (hijria) kuwa ya mapumziko.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa Mtaa wa Kwaboko mara baada ya kutoka msikitini kwa ajili ya Ibada ya sala ya Ijumaa katika Msikiti Kubba uliopo Kwaboko,Mkoa wa Mjini Magharibi leo.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesema hayo katika salamu zake kwa Waislamu baada ya kukamilisha Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika Masjid Kubba, Kwa Boko Mkoa Mjini Magharibi.
Amesema, Dunia iniatambua Kalenda ya Hijria ambapo waislamu hupata fursa ya kuadhimisha mwaka mpya wa kiislamu, hivyo akatumia nafasi hiyo kuipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuja na utaratibu wa kuadhimisha Kalenda hiyo.
Alhaj Dkt. Mwinyi alisema Serikali imeridhia maombi ya waislamu ya kuifanya siku hiyo kuwa ya mapumziko kitaifa kama ilivyo siku ya mwaka mpya wa Miladia.
Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi aliwataka waislamu kuzingatia kwa kina umuhimu wa kufunga siku ya Ashuraa, ikiwa ni funga yenye fadhila kubwa katika mwezi huu wa Muharam.
Nae, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume aliwataka waislamu kuendelea kumuombea Dua Rais Alhaj Dk. Mwinyi kwa kuwa ni kiongozi muadilifu na mwenye kutekeleza kwa vitendo ahadi alizoweka.
Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Hija Suleiman aliwataka waislamu kuendelea kufanya amali njema na kuondokana na maovu, kwa kutambua kuwa mwezi huu wa Muharam ni miongoni mwa miezi minne mitukufu katika uislamu.
Alieleza kuwa kuna fadhila nyingi zinazopatikana katika mwezi huu wa Muharami, ikiwemo ile inayotokana na muislamu kukuthirisha funga , ambapo hupata malipo makubwa.
“Kuna fadhila kubwa kwa kufunga sikukuu hii ya Ashuraa, mja hufutiwa madhambi ya mwaka mzima uliopita,”alisema.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi alipata fursa ya kufika nyumbani kwa Al-marhum Hijjat Akiba Haji Ramadhana Fuoni Wilaya Magharibi B Unguja, aliyefariki dunia nchini Saudi Arabia akishiriki Ibada ya hijja na kuzikwa katika Mji wa Madina.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ya kumuombea marehemu Hajjat Akida Rajab aliyefariki Madina nchini Saudi Arabia, baada ya kumaliza kwa Ibada ya Hijja, ikisomwa na Sheikh Abdalla Talib kushoto kwa Rais na kulia kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria,Utumishi na Utawala Bora, Mhe.Haroun Ali Suleiman, baada ya kutoa mkono wa pole kwa familia ya marehemu Fuoni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo (Picha na Ikulu).
Alhaj Mwinyi aliiomba familia ya marehemu huyo kuwa na mioyo ya subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa mpendwa wao pamoja na kumtakia malazi mema marehemu huyo.