NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na TAMISEMI kupitia Halmashauri zote nchini na kuhakikisha zinaweka mipango ya kukusanya mapato.

Rais Samia amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Chunya -Makongorosi kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 39 iliyofanyika katika uwanja wa Matundasi.
Aidha, Rais Samia amesema mapato yanayokusanywa na Halmashauri yakisimamiwa vizuri yanaweza kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

Vile vile, Rais Samia ameeleza barabara hiyo itafungua fursa za kibiashara kwa wananchi wa Chunya kwani inaunganisha mkoa wa Mbeya na mikoa ya jirani.