Rais Samia aweka jiwe la msingi ujenzi jengo la mama na mtoto Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya

NA MWANDISHI WETU

KUKAMILIKA kwa jengo la kutolea huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kutaongeza idadi ya akina mama wajawazito wanaofika kujifungua katika hospitali hiyo kutoka mama wajawazito 150 kwa sasa hadi kufikia 300 kwa wakati mmoja.
Kauli hiyo imetolewa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Jengo la kutolea huduma za Mama na Mtoto katika Kitengo cha Wazazi Meta.

“Hospitali hii itatoka kulaza akina mama 150 hadi kufikia zaidi 300 kwa kanda nzima, wakina mama watakaokuwa na hali ngumu pia wataletwa hapa,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa jengo hilo limewekewa miundombinu ya kisasa ya kuweza kusaidia utoaji wa huduma bora kwa akina mama wajawazito na watoto huku pamoja na kuweka miundombinu ya kuruhusu wanaume kuwepo katika shughuli hiyo ya kuleta kiumbe duniani.

“Mimi kama mama kazi inayofanywa humu ndani naijua vizuri, naelewa kwamba ni kazi inayohitaji mazingira mazuri sana lakini pia inahitaji faraja na kwa maana hiyo hospitali hii tumeweka vyumba ambavyo mwenza wako atakuwemo humo ndani” amesema Rais Samia

Rais Samia amesema kuwa Serikali inafanya yote haya ili kuokoa Maisha ya Mama na Watoto huku akisema kuwa uwekezaji huo uliofanywa katika Nyanda za Juu Kusini unafanyika katika maeneo mengine nchi nzima.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka jiwe la msingi katika Hospitali hiyo na kumpongeza Rais Samia kwa kuendeleza kazi walioyoianza toka Awamu ya Tano ambapo Serikali ilitoa Shilingi Bilioni 5 kuanza ujenzi wa jengo huku Serikali ya Awamu ya Sita nayo ikiendeleza ujenzi kwa kutoa Shilingi Bilioni 6 kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ambalo jumla limeghalimu Shilingi Bilioni 11.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news