NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Simba Queens baada ya kutwaa ubingwa wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Simba Queens ilishinda taji hilo Agosti 27, 2022 baada ya kuifunga SHE Corporates kutoka Uganda bao moja katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamanzi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Rais Samia ametuma salamu za pongezi na kuwatakia heri katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake itakayofanyika nchini Morocco.
“Nawapongeza wanangu wa Simba Queens kwa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa Wanawake (SAMIA CUP). Mmejenga heshima kwa soka la Tanzania na nchi kwa ujumla.
“Nawatakia kheri katika Ligi ya Mabingwa Afrika (2022 CAF Women’s Champions League) itakayofanyika nchini Morocco,”ameandika Rais Samia.
Awali, mchezo huo ulikuwa mkali na wa kuvutia kutokana na timu zote kujuana vizuri kwani walishakutana katika hatua ya makundi na Simba Queens wakaibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Pamoja na kupata ushindi huo, lakini Simba Queens walikuwa na uwezo wa mabao mengi zaidi kama wangeongeza umakini katika nafasi walizotengeneza.
Mlinda mlango wa SHE Corporates alionesha kiwango bora kwa kuokoa michomo ya washambuliaji ambapo kama asingekuwa makini dhahama kubwa ingewakuta mabingwa hao wa Uganda.
Kiungo mkabaji Vivian Corazone alitupatia bao hilo pekee kwa mkwaju wa penati dakika ya 47 ambalo liliweezesha kubakisha taji katika ardhi ya nyumbani.
Ubingwa huu unawafanya Simba Queens kupata tiketi ya kuiwakilisha Ukanda wa CECAFA katika Ligi ya Mabingwa Afrika na wanakuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufanya hivyo.