NA FRESHA KINASA
MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT), Rhobi Samwelly amesema, shirika hilo halitarudi nyuma kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni katika Mkoa wa Mara ili kuhakikisha watoto wa kike wanaondoka na vitendo hivyo.
Lengo ni kuhakikisha wanapata fursa ya kusoma na kuhitimu kwa ufaulu unaotakiwa kusudi wasonge mbele na waje walete manufaa chanya ya kiuchumi, kulitumikia taifa na kuliletea maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linajishugulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo lina makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara ambapo limekuwa likifanya kazi kwa karibu na Dawati la Jinsia na Watoto wilayani humo, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ikiwemo kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukeketaji, ndoa za utotoni kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Pia,shirika hilo lina vituo viwili vinavyotoa hifadhi kwa wasichana ambao hukimbia ukeketaji kutoka katika familia zao ambavyo ni Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama na Kituo cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama.
Rhobi amesema, vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni vinakiuka sheria za nchi pamoja na haki za binadamu.
Hivyo lazima vitendo hivyo vikomeshwe ili watoto wa kike wawe salama katika kujenga jamii imara inayothamini na kulinda haki na usawa kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
"Hope for Girls and Women in Tanzania pia hatutachoka kupambana na ukeketaji, tutaokoa mabinti na kuwasaidia. Maana kukeketa ni kosa la jinai na ni uvunjifu wa haki za binadamu,"amesema Rhobi.
Ameongeza kuwa, jukumu la kupambana na ukeketaji na ndoa za utotoni linapaswa kuungwa mkono na kila mmoja na kwamba, wanaofanya vitendo hivyo ama kuwalinda wahusika wafichuliwe mbele ya vyombo vya sheria bila kufumbiwa macho kwani wanakwamisha juhudi za Serikali katika kutokomeza vitendo hivyo.