NA DIRAMAKINI
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umewakaribisha wananchi wote kutembelea katika banda lao ili kupata huduma kwenye maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wakulima yanayofanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale maarufu kama viwanja vya Nanenane.
Huduma zinazopatikana katika banda la RITA ni, Usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa watu wote waliozaliwa Tanzania bara, elimu kwa umma kuhusu usajili wa Ndoa na Talaka, Ufilisi na Udhamini pamoja na huduma ya msaada wa kisheria kuhusu masuala ya Wosia na Mirathi.

Maonesho hayo yaliyoanza Agosti Mosi yanatarajiwa kufikia kilele Agosti 8, 2022 ambapo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale maarufu viwanja vya Nanenane mkoani Mbeya na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.