NA DIRAMAKINI
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema, huenda mwaka ujao mipango ikienda vizuri ikaona namna ambavyo itawezesha upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma elimu ya ufundi stadi nchini.
Prof. Adolf Mkenda ambaye ni waziri wa wizara hiyo ameyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari juu ya Mwelekeo wa Wizara, Vipaumbele na Maeneo ya Kimkakati katika Utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.
"Vile vile pamoja na hayo mtakumbuka Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha na Mipango ametangaza kutenga Shilingi Bilioni 8 kupitia mfumo wa TASAF kwa ajili ya kusaidia wanafunzi kusoma.
"Pia tumeongea na Benki ya NMB ambayo nayo imetenga Shilingi Bilioni 200 sasa hizi Bilioni 200 zitatolewa kama mkopo na tumeweza kupata riba ndogo asilimia 9 kwa wale ambao wanapitisha mapato yao kupitia NMB akitaka kwenda kusoma chuo cha Ufundi VETA na kadhalika unaweza ukachukua mkopo dhidi ya kile ambacho unakipata kinapitia NMB.
"Mkopo huu wa shilingi Bilioni 200 utawanufaisha wale ambao pengine wanalipwa mshahara unapitia NMB halafu kwa makubaliano hayo utapata mkopo
"Tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba tunaongeza upatikanaji wa elimu hasa ya ufundi ambapo kwa mwaka huu tunaotekeleza sasa hivi mikopo ya elimu ya juu bado hatujaipeleka kwenye elimu ya ufundi, ninaamini kwamba bajeti ijayo tutajipanga kuhakikisha kwamba tunatoa fursa ya watu kwenda kusoma elimu ya ufundi na VETA kwa sababu ni muhimu sana,"amesema Prof. Mkenda.