NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa Serikali inatarajia kuanza kuruhusu magari kupita juu ya daraja jipya la Wami, lililopo mkoani Pwani ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri huyo wakati akikagua hatua za maendeleo ya daraja hilo ambapo pamoja na mambo mengine amemtaka mkandarasi kukamilisha kazi ndogo ndogo zilizobakia katika daraja hilo ili kurahisisha matumizi salama ya watumiaji wa daraja hilo.
"Hadi sasa kazi zinaendelea vizuri, ni matumaini yangu hadi kufikia tarehe 20 Septemba, mtakuwa mmeshakamilisha kazi zilizobaki ili mimi niweze kuruhusu magari kupita,"amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameeleza kuwa mradi huo ambao umefikia asilimia 86 katika utekelezaji wake unajumuisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 513.5 pamoja na ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 3.8.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya kimkakati na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji nchini.
Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani, Mhandisi Heririsper Mollel, ameeleza kuwa kwa upande wa ujenzi wa daraja mkandarasi amekamilisha ujenzi wa sehemu ya chini ya daraja kwa asilimia 100 na sehemu ya juu amekamilisha tabaka la juu la lami mita 256 kati ya mita 513.5 ambayo ni sawa na asilimia 50 ya urefu wa daraja.
Ameongeza kuwa, kazi nyingine zilizokamilika ni ujenzi wa makalvati makubwa matatu na madogo saba na uwekaji wa mabomba 188 ya maji kati ya 206 ambayo ni sawa na asilimia 91.
Kuhusu ujenzi wa barabara unganishi Eng. Heririsper amesema kuwa hadi sasa kilometa 3.4 za ujenzi wa tabaka la lami la chini zimekamilika.