Serikali yatenga Bilioni 1.5/- za ujenzi miundombinu ya Chuo cha Mafunzo ya Jeshi la Zimamoto

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imetenga kiasi cha sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Chuo cha Mafunzo ya Jeshi la Zimamoto kilichopo eneo la Chogo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga pamoja na kuendelea kuend Lea kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Wahitimu wa mafunzo ya awali Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiwa tayari kukaguliwa na Waziri Masauni.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni wakati akifunga mafunzo ya awali ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kozi namba 01, 2022 katika chuo cha Chogo juzi na kusema serikali imepanga kuimarisha jeshi ili kuwatumikia wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema serikali imeendelea kuboresha pia maslahi ya Maofisa na Askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na kwamba badala ya kukatwa posho wakiwa mafunzo kwa sasa serikali imebeba mzigo huo na katika kutekeleza hilo, katika bajeti ya 2022/23 kiasi cha sh milioni 420 zimetengwa kwenye bajeti ya Jeshi.

"Pamoja na jitihada hizi zinazochukuliwa na serikali, tutambue kwamba nasi tuna jukumu kubwa la kuwajibika kwa uaminifu na uadilifu kuwatumikia wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla,"amesema Masauni.

Aidha, Masauni ametoa pongezi kwa wahitimu wa mafunzo hayo na kusema inawapasa watambue majukumu na mipaka yao kwakuwa wamebeba dhamana kubwa ya kuokoa maisha na mali za Watanzania, huku alisisitiza wananchi wote kujiandaa kuhesabiwa siku ya sensa ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni akiwa jukwaani tayari kwa kukagua gwaride la jeshi la wahitimu wa mafunzo ya awali ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kozi namba 01/ 2022 katika Chuo cha jeshi hilo

"Nawasihi sana muende kutekeleza majukumu yenu ipasavyo, Wizara hatavumilia vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu na hatua kali sana zitachukuliwa bila kuwa na huruma, nakuagiza Kamishna Jenerali, endelea kusimamia nidhamu ya Jeshi kwa Maofisa na Askari wote pamoja na Hawa ambao wanahitimu mafunzo siku ya leo" amesema.

"Lakini pia natoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla wao kuwa tayari kushiriki na kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi ambayo utafanyika siku chache zijazo kwa maana ya Agosti 23 mwaka huu,"amesisitiza.

Awali akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Paul Ekidungu amesema katika mafunzo hayo wamejifunza mambo mengi kwa nadharia na vitendo na kuwafanya kuwa wabobezi katika jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kwamba yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, maarifa na ufanisi mkubwa.

"Licha ya kwamba waswahili wanasema mwanzo ni mgumu, lakini sisi tutajitahidii kadri tuwezavyo kutekeleza vema majukumu tutakayopangiwa kwa maslahi napana ya jeshi letu na Taifa kwa ujumla,"amesema Ekidungu.

Aidha, Ekidungu amesema mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Kamishna wa jeshi, Utawala na Fedha Mbaraka Semwanza Januari 28 mwaka huu na yamechukua takribani wiki 32 sawa na miezi nane, ambapo waliohitimu ni wanafunzi 400, wakiwemo wanawake 114 na wanaume 286.
Waziri Masauni akitoa vyetu vya ushindi kwa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao.

"Pamoja na mafanikio mengi tuliyoyapata kwenye mafunzo, tumekutana na kero mbalimbali zikiwemo, upungufu wa mabweni ya wanafunzi, madarasa pamoja na mabwalo ya kulia chakula, ukosefu wa chemba za Moshi, vikwazo mbalimbali, mabwawa ya kuogelea pamoja na upungufu wa wataalamu wa afya"

"Lakini pia kuna upungufu wa vifaa tiba vya kisasa na madawa katika hospitali tunayotumia, ukosefu wa zahanati ya chuo kwani tunatumia zahanati ya kijiji ambayo kimsingi haitoshelezi mahitaji" amebainisha.

Hata hivyo amesema chuoni hapo hakuna nishati ya umeme na kwamba serikali inatumia garama kubwa kwa ajili ya kuzalisha umeme ambao haukidhi mahitaji yao kwakuwa inawashwa kulingana na upatikanaji wa mafuta, lakini pia kuna ukosefu wa maji safi na salama.

"Kutokana na miundombinu ya maji kutokamilika, chuo kinatumia garama kubwa kutafuta maji nje ya chuo hasa katika vijiji vya jirani ambako kunapatikana maji ya visima ambayo kimsingi siyo salama, lakini pia kuna upungufu wa vitanda vya wanafunzi" amebainisha.

Sambamba na hayo, wahitimu hao walimuomba Waziri Masauni kupitia serikali kuangalia namna ya kuweza kuwatatulia kero hizo ambapo pia walisema wamejinga kikamilifu kwenda kutoa ushirikiano katika jamii na wameshajiandaa kuhesabiwa ifikapo Agosti 23 kwenye sensa ya watu na makazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news