NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Chakula na Dawa ya Saudia (SFDA) imepiga marufuku kwa muda uagizaji wa nyama ya kuku, mayai na bidhaa zinazohusiana kutoka eneo la Wielkopolskie nchini Poland.
Hatua ya mamlaka hiyo imekuja baada ya kupokea taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), kufuatia milipuko ya homa kali ya mafua ya ndege, pamoja na madhara yake huko Wielkopolskie.
Kwa mujibu wa SFDA, imeweka marufuku ya muda ya bidhaa hizo ili kuhakikisha mlipuko huo wa homa ya mafua hauenei nchini humo.
Mamlaka hiyo pia imeweka masharti kwamba mchakato huu pia unazingatia mahitaji na vidhibiti vya afya na vipimo vya kawaida vilivyoidhinishwa, cheti cha afya kilichotolewa na mamlaka rasmi kilichoidhinishwa na Poland kuthibitisha kuwa bidhaa husika haina virusi.
Hayo yanajiri ikiwa mlipuko wa ugonjwa wa mafua ya ndege (Bird Flue) uliripotiwa kujitokeza nchini Poland tangu mwishoni mwa mwaka 2019, hali iliyopelekea baadhi ya nchi kuweka zuio la uingizaji wa bidhaa za nyama ya ndege (poultry meat and poultry products) kutoka nchi hiyo.
Katika moja ya taarifa iliyoripotiwa na Afisa Mkuu wa Mifugo kupitia Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Miji nchini Poland ilitaja kuthibitishwa juu ya hali ya mlipuko wa mafua ya ndege iliyotokea mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2019.