NA JOHN MAPEPELE
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia upya kanuni kwa kuwashirikisha wadau wote wa Sanaa nchini Tanzania ili ziweze kuainisha bayana mfumo mzuri wa ufanyaji kazi unaowashirikisha wasanii binafsi, vyama, na mashirikisho ya Sanaa.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa mfano wa hundi ya milioni 30 ikiwa ni pongezi ya serikali kwa wachezaji wote walioshiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo Agosti 13, 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa rasmi ya namna bora ya ya kusimamia HAKIMILIKI na Mirabaha kwa wasanii nchini kutoka kwa Kamati aliyoiteua Julai Mosi mwaka iliyoongozwa na Victor Tesha.
“Mfumo huu utasaidia kuwatambua wasanii wote nchini na kuweza kuwahudumia kwa urahisi kwani mfumo uliopo sasa unatoa nafasi ya kila msanii kujitafutia riziki mwenyewe kitu kinachofanya wasanii wengi kukosa umoja na kuzalisha migogoro isiyokuwa na tija,”amesisistiza Mhe. Mchengerwa.
Pia, ameliagiza BASATA kufanya mapitio na usuluhishi katika migogoro ya wasanii, ikiwa ni pamoja na kuandaa dawati la ushauri wa kisheria kuhusu mikataba na masuala ya sanaa.
Aidha, ameongeza kuwa masuala yanayohusu usimamizi wa hakimiliki ni mtambuka na yanahusisha taasisi nyingi za Serikali na nyakati fulani zenye maslahi pingani, hivyo mapendekezo yaliyotolewa na kamati ya kuwa na mfumo bora wa uendeshwaji wa Taasisi ya Hakimiliki yatazingatiwa na Serikali ili kurekebisha mnyororo mzima wa kazi za sanaa nchini na hivyo kupelekea kutengeneza sekta ya sanaa iliyo na nguvu zaidi katika ukanda wa Afrika na dunia kwa ujumla.
Ameongeza kuwa, wizara ina mkakati wa uwezeshaji kwa kujenga majukwaa ya kuendeleza kazi za wasanii, kuwekeza katika “Digital Platform” ili wasanii wapate uwanja wa kuuza na kutangaza bidhaa zao.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea taarifa ya kamati ya HAKIMILIKI kutoka kwa Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Pia kuratibu na kuweka kanuni mahususi kwa lengo la kuendeleza kuongeza thamani za kazi zote za Sanaa.
Wakati huo huo Waziri Mchengerwa amekabidhi bonasi ya shilingi milioni 30,000,000 itakayogawanywa kwa wachezaji na benchi la ufundi lote lililoshiriki katika michezo ya Jumuiya ya Madola pamoja na kuwapatia fedha wachezaji watatu walioshinda medali kwenye mashindano hayo.
Wachezaji hao ni Nahodha wa timu ya Tanzania Bw. Felix Simbu aliyetwaa medali ya fedha na kunyakua dola 7500 na Mabondia Bw.Yusufu Changalawe na Bw.Kassim mbundwike waliotwaa medali za shaba ambao Serikali iliwapatia dola za kimarekani 5000 kila mmoja.
Katika kuhakikisha timu za Tanzania zinaendelea kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, Mhe. Mchengerwa ameielekeza Idara ya Michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuanza maandalizi haraka ya kuandaa Timu za Taifa kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya ALL AFICAN GAMES yatakayofanyika nchini Ghana katika mji wa Accra kuanzia tarehe 14 -18 Agosti 2023.