NA GODFREY NNKO
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema kuwa, awamu ya kwanza ya udahili kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2022/2023 imekamilika.
Prof. Charles D.Kihampa ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ameyabainisha hayo leo Agosti 24, 2022 jijini Dar es Salaam ambapo majina ya waliodahiliwa katika awamu hii yanatangazwa na vyuo husika.
Amesema, katika Awamu ya Kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 106,295 wametuma maombi ya kujiunga katika vyuo 76 vilivyoidhinishwa kudahili.
Aidha, jumla ya programu 757 zimeruhusiwa kudahili ikilinganishwa na programu 724 mwaka 2021/2022. Vilevile kwa upande wa nafasi, mwaka huu kuna jumla ya nafasi 172,168 ikilinganishwa na nafasi 164,901 mwaka uliopita.
"Hili ni ongezeko la nafasi 7,267 sawa na asilimia 4.4 katika programu za Shahada ya Kwanza. Pia katika Awamu ya Kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 75,163 sawa na asilimia 70.71 ya waombaji wote walioomba udahili wameshapata udahili vyuoni.
"Mwenendo wa udahili wa Awamu ya Kwanza kwa kipindi cha miaka mitano (2018/2019 hadi 2022/2023) unaonesha ongezeko kubwa la waombaji ikiashiria ongezeko la wahitimu wa Kidato cha Sita na wale wa Stashahada,"amesema Prof.Kihampa.
Pia amesema, idadi ya waliodahiliwa katika Awamu ya Kwanza ya Udahili kwa kipindi cha miaka mitano (2018/2019 hadi 2022/2023) nayo imekuwa ikiongezeka.
Mchanganuo wa mwenendo wa udahili kwa Awamu za Kwanza kwa kipindi cha miaka mitano umeainishwa hapa chini;
Prof.Kihampa amesema, waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia leo Agosti 24 hadi Septemba 6, 2022 kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.
"Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika.
"Uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia wakati wa kuomba udahili. Orodha ya majina ya waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja imewekwa kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz),"amesema Prof.Kihampa.
Awamu ya Pili
Wakati huo huo,TCU imetangaza kuwa Awamu ya Pili ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2022/2023 imeanza rasmi leo Agosti 24 hadi Septemba 6, 2022.
"Tume inasisitiza kuwa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo
wanavyovipenda.
"Tume inaelekeza Taasisi za Elimu ya Juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi. Aidha, waombaji na vyuo wanahimizwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa Awamu ya Pili kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyoko katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz),"amesema Prof.Kihampa.
Prof.Kihampa ametoa wito kwa waombaji udahili wa Shahada ya Kwanza kuzingatia masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja na maombi yao yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.
Amesema, kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha,vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.
"TCU inawaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya Elimu ya Juu hapa nchini,"amesema Prof.Kihampa.