NA DIRAMAKINI
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewahimiza Watanzania kujitokeza kuhesabiwa wote ifikapo Agosti 23, 2022 kupitia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, kwani hilo ni zoezi muhimu katika upangaji wa maendeleo ya nchi.
Pia amesema, takwimu zinaonesha mpaka sasa asilimia 98 ya Watanzania wanafahamu kuhusu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 23, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mheshimiwa Nape Nnauye katika Tamasha la Uhuru Fm Sensa Marathon lililofanyika kwenye uwanja wa Majengo huko Mtama mkoani Lindi.
Amesema, huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya,elimu na huduma nyingine,zitaboreshwa zaidi iwapo Serikali itakuwa na takwimu sahihi za wananchi wake.
Akizungumzia watu wenye mahitaji maalumu, Mheshhimiwa Nape kwa niaba ya Waziri Mkuu amesema watu, hao ni lazima wahesabiwe ili nao takwimu zao zipatikane,na wahudumiwe vizuri na Serikali.
Naye Mheshimiwa Salma Kikwete ambaye ni Mbunge wa Mchinga mkoani Lindi amesema, wabunge wa mkoa huo na wananchi wao wamejipanga kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi huku akisisitiza zoezi hilo mwaka huu litafanyika kisasa zaidi,tofauti na miaka iliyopita.