NA MWANDISHI WETU
MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Neville Meena amesema, sheria ya habari kuielekeza mahakama kutoa hukumu kwa mujibu wa watunga sheria, inaiweka tasnia hiyo njia panda.
Mahakama haipaswi kufungwa na sheria ya habari katika kutoa hukumu yake kulingana na uzito wa kosa alilotenda mwandishi wa habari.
Ameyasema hayo Agosti 29, 2022 wakati akizungumza katika Kipindi cha Sun Down kinachorushwa na Radio Ukweli (Ukweli FM) mjini Mrorogoro.
Amesema, sio sawa mahakama kulazimishwa na sheria kumfunga mwandishi miaka mitatu ama zaidi hata pale kosa lake linaweza kumalizwa kwa kuonywa ama kifungo chini ya miaka hiyo.
Meena amesema, baadhi ya vipengele vya Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, vinailazimisha mahakama kutenda kwa matakwa ya watungaji wa sheria hiyo.
“Tusitunge sheria kwa ajali ya kuilazimisha mahakama kutenda kwa mujibu wa yaliyopo mioyoni mwa watunga sheria,”amesema Meena.
Akifafanua kauli yake amasema, hatua ya sheria kumuelekeza hakimu kutoa kifungo kisichopungua miaka mitatu, ni kumlazimisha asitoe hukumu chini ya kiwango hicho.
“Inawezekana hakimu akaona kosa la mwandishi linahitaji kifungo cha miaka miwili au mmoja au miezi sita na pengine miezi mitatu ama kifungo cha nje.
“Lakini kutokana na sheria hii, hakimu hawezi kutoa kifungo nje ya kile kilichoelezwa na sheria, sasa huku ni kulazimisha kila aliyetenda kosa kwenye tasnia ya habari afungwe sio chini ya miaka mitatu. Jambo hili tunaona lina ukakasi,”amesema Meena.