VIONGOZI WA DINI YA KIISLAMU NCHINI WAELEZA DHANA YA SENSA NA KUWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KUHESABIWA

NA DIRAMAKINI

VIONGOZI wa dini ya Kiislamu nchini wameungana na serikali pamoja na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuunga mkono zoezi la Sensa ya Watu na Makazi nchini inayotarajiwa kufanyika mnamo Agosti 23, 2022.
Kauli za viongozi hao inakuja siku chache kabla ya zoezi la kuhesabiwa kwa wananchi wote nchini ambapo elimu na hamasa imeendelea kutolewa kwa wananchi kushiriki ipasavyo licha ya kuwepo kwa elimu potofu kutoka kwa watu wachache juu ya dhana ya Uislam kutokubali kuhesabiwa.

"Vitabu vitakatifu vinatueleza kuwa katika sisi kila kitu unachokiona vimeumbwa katika mpango, maana ya mipango ni uratibu mzuri wa masuala mbalimbali, na zoezi la Sensa linaafikiana kabisa na dhana ya mipango iliyo katika kitabu chetu tukufu,"amesema Sheikh Mussa Yusuph Kundecha.

Naye Sheikh Khamis Mataka Mwenyekiti Halmashauri Kuu ya Taifa Bakwata ameongezea kwa kusema, "Sensa ni nyenzo ya kupanga maendeleo, haiwezekani kupanga maendeleo ya watu usiowafahamu idadi, hata mtume wetu Muhammad SAW alifanya Sensa alipotaka maswahaba wampe hesabu ya watu ambao wametamka shahada".

Viongozi hao ambao wameelezea chimbuko la zoezi la Sensa kwa dini ya Kiislamu wametaja namna sensa iliratibiwa kwa viongozi wakuu wa dini hiyo enzi na enzi na kwamba ina manufaa hata sasa kwa nchi yetu.

Sheikh Hillary Makarani maarufu Sheikh Kipoozeo amewakumbusha waumini wa dini ya Kiislam kuwa inatakiwa hata chakula kipimwe, na kipimo ndio maana ya dhana ya Sensa.

"Sensa si jambo geni katika Uislam, Mtume SAW alituasa tupime mpaka vyakula ili tufanye vitu kwa vipimo, hivyo watanzania wajitokeze kwa wingi kuhesabiwa kwa sababu za maendeleo na tumuunge mkono Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan,"amesema Sheikh Kipoozeo. TAZAMA VIDEO HAPA;
Viongozi wengine wa dini ya kiislam ambao wameungana kwa kauli moja katika zoezi la Sensa Agosti 23, ni pamoja na Sheikh Mohammed Idd Mohammed, Imam na Mwenyekiti wa Taasisi ya Al Risaalah Islamic Foundation pamoja Tariq Othman Twaha ambao kwa pamoja wamewaasa waislam wote kukaa mbali na kauli na upotoshaji juu ya zoezi la Sensa na kujitokeza kuhesabiwa bila kukosa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news