NA DIRAMAKINI
WADAU wa michezo nchini wameonesha kuguswa na namna ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anavyoshiriki kukuza vipaji vya Watanzania na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha soka la Tanzania linastawi ili liweze kutoa ajira ndani na nje kwa wananchi wake.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 16, 2022 na wadau hao katika mkutano maalum ulioratibiwa na Watch Tanzania ukiangazia juu ya tathimini na matarajio ya wadau wa soka kuhusu mwenendo wa usajili wa wachezaji kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2022/23.
MH.MOHAMMED MCHENGERWA, WAZIRI WA SANAA,UTAMADUNI NA MICHEZO
"Toka Rais wa Awamu ya Sita Mhe.Rais Samia alivyoingia madarakani ameona haina sababu ya kujiweka nyuma katika kusimamia na kukuza vipaji vya Watanzania, ndio maana serikali yetu sikivu inajitahidi kadri iwezavyo kusapoti michezo yote hasa miguu na kuitangaza nchi;
"Ndani ya awamu hii tumejipanga kuhakikisha tunaboresha viwanja vyetu, tunajenga academia 56 yaani kila mkoa kutakuwa na academia mbili, hiki ni kitu kikubwa hakijawahi tokea tangu tupate uhuru,"amesema Mheshimiwa Waziri Mchengerwa.
WALLACE KARIA, RAIS WA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MGUU TANZANIA ( TFF)
"Mfumo wetu wa kufungua ligi na ngao ya hisani kuchezwa na timu nne ni mfumo kutoka Spain, hii ilitokana na maamuzi ya kikao kule Arusha na ipo kwenye kanuni zetu;
"Huwezi kuwa na mapenzi ya mpira wa miguu ukawa kiongozi wa boxing, hivyo kila kiongozi ana timu yake na mapenzi yake, hivyo mimi timu yangu ni Coast Union na sio Simba, Kipindi cha nyuma nilikwenda kwenye Tamasha la Simba Day kumwakilisha Rais Malinzi,"amesema.
KIDAO WILFRED, KATIBU MKUU SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
"Tumekuwa na maboresho mbalimbali katika kanuni zetu na tumejitahidi kushirikisha vilabu vyote, wadau mpaka vyombo vya habari kupata maoni yao kwa mstakabadhi bora wa ligi yetu;
"Wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu wameongeza thamani kwa kiwango kikubwa, imefika hatua mpaka vilabu vikubwa nje ya Tanzania wananunua wachezaji kutoka kwenye ligi yetu ndio maana tukaamua kuja na kanuni ya kuchezesha wachezaji 12 wa kigeni na sio nane kama ilivyokuwa zamani;
NEEMA MSITHA, MTENDAJI MKUU WA BARAZA LA MICHEZO TAIFA (BMT)
"Baraza linahakikisha baada ya vyama vya michezo kuwasilisha katiba na kanuni zao, je wanazifuata hizo katika na kanuni hizo;
"Baraza la michezo Taifa linahakikisha kila kilabu kinajenga viwanja vyake, kwani viwanja vinaongeza thamani na kinaongeza kipato kama viwanja vikitumika,"amesema.
RIZIKI JUMA MAJALA, MSAJILI WA VYAMA VYA MICHEZO NCHINI
"Kwa mujibu wa kanuni zetu tunatoa adhabu ya kumfutia uongozi, kusimamisha na kumwondolea tuzo kiongozi yeyote atakayekwenda kinyume na kanuni na katiba ya vyama;
"Vyama na vilabu vya michezo vinawajibu kulipa Ada kila mwaka japo inakuwa inabadilika kutokana na thamani ya shillingi,"amesema.
MHANDISI HERSI SAID, RAIS WA KLABU YA YANGA
"Ndani ya msimu huu wa 2022-2023 kama Timu ya Yanga tumejipanga vyema kuhakikisha tunafanya vizuri na kuchukua makombe matatu na kuongeza la mapinduzi na kufika hatua ya makundi katika ngazi ya champions league"
"Katika kufanya vizuri tumefanya usajili wa kutosha kuweza kufika mbali zaidi ndio maana tumesajili wachezaji wenye uzoefu wa kutosha kushiriki mashindano ya Afrika,"amesema Mhandisi Said.
AHMED ALLY, MSEMAJI WA SIMBA SC
"Wanasema kuteleza sio kuanguka kukosa ngao ya jamii sio kukosa ubigwa, hivyo sisi kama Simba tumeleta watu sahihi, kwani walipotoka kwenye vilabu vyao walifanya makubwa hivyo tunaamini wataitumikia klabu ipasavyo;
"Wachezaji tuliowaleta hatujaja kuwalea wala kuwafunza bali kuongeza chumvi katika kikosi chetu na tunaamini tutafanya vizuri zaidi kwenye ligi ya ndani na hasa michezo ya kimataifa,"amesema.
MASAU BWIRE, AFISA HABARI WA RUVU SHOOTING STARS
"Viongozi wa TFF wamefanya makubwa mno hivyo kila mdau wa soka awapongeze na kuwasifia kwani soko letu linatazwa mpaka nje ya mipaka ya Tanzania hivyo wapewe pongezi nyingi sana;
"Misimamo ya klabu yetu ni uzalendo kwanza hivyo hatutarajii kusajili mchezaji yeyote nje ya Tanzania hivyo sisi wachezaji wetu wote wanatoka hapa hapa hivyo wakutane na hao wageni kusudi tujue nani bora zaidi,"amesema Masau Bwire.