NA DIRAMAKINI
WACHEZAJI wa Klabu ya Simba SC leo wakiwa katika maandalizi ya mwisho kuelekea tamasha kubwa la SIMBA DAY ambapo wanatarajiwa kucheza dhidi ya Mabingwa wa Soka Ligi Kuu ya Ethiopia, klabu ya St. George SC wametumia muda wao kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi la Sensa la Agosti 23, 2022.
Wachezaji hao wakiongozwa na Kapteni John Bocco, wameungana na
Shomari Kapombe, Aishi Manula, Erasto Nyoni na wazawa wengine kumuunga
mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa wako tayari kuhesabiwa.
"Sisi
wachezaji wa Simba SC tunapenda kuwahamasisha watanzania wajitokeze
kuhesabiwa kwani ni muhimu kwa maendeleo na mipango ya nchi yetu,
tumuunge mkono Rais Samia katika zoezi hili,"amesema Shomari Kapombe
Beki wa kulia wa Simba.
Naye Clatous Chama amewaasa watanzania kujitokeza kuhesabiwa kwani zoezi hilo hufanyika nchi zote ili kuweka utaratibu mzuri wa maendeleo ya nchi.
Chama anaungana na wachezaji wengine wa kigeni ikiwemo Joash
Onyango pamoja na Victor Akpan kuwaasa watanzania kujitokeza kuhesabiwa
tarehe 23 Agosti, 2022.
Septemba 14, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakati akizindua rasmi Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 alisisitiza faida lukuki zitokanazo na sensa hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizindua rasmi Mpango wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Septemba 14, 2021 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia alisema lengo la Mkakati huo ni kupata taarifa sahihi za idadi ya watu waliopo nchini ikiwemo jinsia, elimu, afya na hali za ajira ili kuwa na takwimu sahihi zitakazoiwezesha Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu wake.
“Taarifa za Sensa zitatusaidia kujua idadi ya watu wapi walipo, elimu zao, afya zao, hali ya ajira zao pamoja na makazi yao, pia zitatusaidia kujua ongezeko la watu wetu ili tuandae Sera ya Taifa na kujua mgawanyo wa rasilimali kwa uwiano sawa kwa wananchi wetu,” alisisitiza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema, haiwezekani kupeleka huduma kwa wananchi wa eneo fulani kama haijulikani idadi ya watu katika eneo husika ambapo amewataka wananchi wote wakaolala ndani ya mipaka ya Tanzania usiku wa kuamkia siku ya sensa kushiriki zoezi hilo.
Pia, Rais Samia alisema, taarifa za sensa hutumika pia kwa watafiti wengi wa ndani na nje ya nchi katika shughuli zao mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo ya kijami, kisiasa na kiuchumi.
Kufuatia hatua hiyo, Rais Samia alitoa wito kwa viongozi mbalimbali nchini wakiwemo viongozi wa dini, kuhakikisha wanawahamasisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika zoezi la sensa litakalofanyika Agosti 23, 2022.