Wageni wanaokomba fedha za watu ATM nchini Saudi Arabia mikononi mwa DPP

NA DIRAMAKINI

ZAIDI ya raia wa kigeni 10 nchini Saudi Arabia wanachunguzwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kwa tuhuma za kujihusisha na genge la uhalifu, ulaghai na wizi kupitia mashine za ATM.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Saudi Arabia, tayari hati ya kuwakamata watuhumiwa hao imetolewa ili upelelezi ukikamilika waweze kupewa haki yao kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.

Chanzo rasmi kutoka Ofisi Mwendesha Mashtaka ya Umma kilisema kuwa, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa genge hilo linajumuisha wahamiaji wanne na wengine sita ambao ni wavunjaji wa sheria ya ukaazi nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa ni kwamba, watuhumiwa hao walikuwa wakiwatapeli watumiaji wa mashine za ATM kwa kuwafuata ili kusaidia kukamilisha taratibu zao za kibenki wanapofika katika mashine hizo.

Chanzo hicho kilisema kuwa, matapeli hao walitumia mbinu zao za kitapeli kupata namba za siri za watumiaji wa mashine za ATM, kisha kubadilishana kadi za benki za wahanga hao bila wao kujua.

Aidha, baada ya kufanikisha mchezo huo mchafu wamekuwa wanatumia tena kadi na kuiba pesa katika akaunti hizo za benki ili kuzitumia kwa manufaa yao.

Chanzo hicho, kwa mujibu wa SAUDI GAZETTE kilidokeza kuwa, taratibu za upelelezi dhidi ya washtakiwa hao zitakamilika, kisha kesi zitapelekwa katika mahakama yenye dhamana, zikitaka wapewe adhabu kali.

"Ni muhimu na ni lazima kwa kila mtu kuwa makini na kuchukua tahadhari na kutokuwa wema katika kuwaamini wengine katika kutumia huduma za kibenki," chanzo hicho kilisema, huku kikiwaonya kila mtu kutoshirikisha taarifa zao za benki na maelezo ya miamala ya fedha na wengine.

Aidha chanzo hicho kiliongeza kuwa, "Tabia au shughuli yoyote inayohusisha ulaghai wa kifedha au unyonyaji na udanganyifu wa wengine inachukuliwa kuwa tabia inayohitaji uwajibikaji mkali,"chanzo hicho kimeongeza.

Hatua

Ripoti za hivi karibuni, zinaonesha kuwa, wimbi la wizi wa fedha katika mashine za kutolea fedha (ATM) katika mataifa mbalimbali duniani limeshika kasi kutokana mbinu nyingi chafu ambazo zinatumiwa na wahalifu.

Aidha, kwa kulibaini hilo, Benki Kuu nyingi ambazo ndizo zenye mamlaka za kusimamia benki na sekta ya fedha katika kila Taifa zimekuwa zikitoa ushauri wa kitaalamu kwa wamiliki wa benki ikiwemo kuziagiza kuweka kifaa cha umeme (electronic chip) kwenye kadi zao za ATM ambazo si rahisi kughushiwa.

Mara nyingi,wizi kama huo huwa unatokea wakati mtu anaweka nywila yake kwenye ATM, kwani kuna watu huweka kamera ambazo husoma na namba hizo kufanikiwa kuzipata kisha kufanya wizi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news