Wazalishaji wa bidhaa za mbogamboga,matunda Tanzania kunufaika na soko la Ulaya

NA MWANDISHI WETU

TANZANIA imejumuishwa kwenye orodha ya nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) zitakazonufaika na utekelezwaji wa Programu mpya ya Fit for Market Plus inayolenga kuwajengea uwezo wajasiriamali na wale wote wanaojihusisha na mnyororo mzima wa uongezaji thamani katika mazao ya kilimo, hususani mbogamboga na matunda ili waweze kuzalisha mazao na bidhaa za kilimo zinazokidhi viwango na mahitaji ya soko, hususan la Umoja wa Ulaya.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 1, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, programu hiyo inayotekelezwa na taasisi ya COLEACP kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya inazingatia Mkakati wa Umoja huo ujulikanao kama Farm to Fork Strategy unaolenga kudhibiti ubora wa bidhaa za mazao ya kilimo zinazoingia kwenye soko kuanzia shambani mpaka zinapomfikia mlaji wa mwisho.

Wizara inatoa wito kwa wadau wote wanaojihusisha na mnyororo wa uongezaji thamani katika mazao ya kilimo cha mbogamboga na matunda kuchangamkia fursa kwa kujitokeza kwa wingi kuwasilisha maombi yao ya kunufaika na utekelezwaji wa programu hii.

Wadau hao ni pamoja na kampuni na vikundi vinavyojihusisha na uzalishaji na uuzaji wa mazao ya mbogamboga na matunda; taasisi zinazojihusisha na utoaji mafunzo na ushauri wa kitaalamu kuhusu kilimo cha mbogamboga na matunda; mamlaka zenye dhamana ya usimamizi wa afya ya mimea; na taasisi za utafiti katika kilimo cha mbogamboga na matunda.

Kwa maelezo zaidi kuhusu namna ya kunufaika na utekelezwaji wa programu hii, wadau wanashauriwa kutembelea tovuti ya COLEACP:https://www.coleacp.org/current-programmes/fit-for-market-plus/.

Wanaweza pia kuwasiliana moja kwa moja na COLEACP kupitia barua pepe support@coleacp.org.

Kupatikana kwa fursa hiyo ni jitihada za Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji katika mikakati yake ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ambao unawahimiza pia wadau kutembelea tovuti: www.be.tzembassy.go.tz ili kupata taarifa zaidi kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye eneo la uwakilishi la ubalozi huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news