Waziri Dkt.Mabula awaonya viongozi wanaojivika madaraka ya kugawa ardhi

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa onyo kwa viongozi wa vijiji na vitongoji kuacha mara moja kujivika madaraka na kuvunja sheria za ardhi kugawa ardhi kinyume na sheria na kusababisha uvamizi kwenye maeneo yenye milki za watu wengine.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Mapinga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani alipokwenda kutoa na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi katika eneo la Mapinga tarehe 10 Agosti 2022.

Dkt Mabula ametoa onyo hilo leo tarehe 10 Agosti 2022 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati akitoa na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi katika eneo la Mapinga.

Taarifa hiyo iliyokabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge inafutia kuundwa kwa Kamati ya kuchunguza migogoro ya ardhi katika eneo la Mapinga wilayani Bagamoyo.
Sehemu ya wananchi wa Mapinga wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) alipokwenda kukabidhi na kutoa taarifa ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi eneo la Mapinga tarehe 10 Agosti 2022.

Katika taarifa yake ya uchunguzi kamati ilibaini mambo 11 yaliyochangia uwepo wa migogoro katika eneo la Mapinga ikiwemo viongozi kujivika madarala kinyume cha sheria kwa kugawa ardhi isivyo halali ambapo viongozi hao wamediriki kugawa hata maeneo yenye milki za watu wengine na kusababisha migogoro ya uvamizi.

Aidha, kupitia taarifa hiyo baadhi ya viongozi wamekuwa wakidiriki kughushi nyaraka ama mihutasari ya ugawaji ardhi kwa kutumia majina ya viongozo wa zamani na kwa makusudi walishuhidia mauziano ya ardhi mara mbili katika ardhi moja kwa lengo la kujipatia fedha.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Taarifa ya Uchunguzi wa Migogoro ya Ardhi katika eneo la Mapinga Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaji Abuubakar Kunenge alipokwenda kutoa na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi kwenye eneo la Mapinga wilayani Bagamoyo tarehe 10 Agosti 2022.

Pia kamati ilibainni kuwepo magenge ya uhalifu yanayovamia ardhi za wananchi na kutumia hila za kuanzisha mashauri mahakamani huku wakiendelea kuuza maeneo hayo jambo lililosababisha madhara makubwa katika utekelezaji wa uamuzi wa mahakama.

"Imebainika uwepo wa wavamizi kukimbilia kufungua mashauri mahakamani wakiwashitaki wamiliki halali wa ardhi lengo likiwa kuwazuia wamiliki kuingia kwenye maeneo yao huku wavamizi wakiendelea kuuza na kuendeleza maeneo hayo" alisema Waziri wa Ardhi Dkt Mabula.

Dkt.Mabula amemuelekeza MsajIli wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Stela Tullo kuanzia Septemba 2022 kufanya program maalum ya kupunguza mlundikano wa mashauri ya ardhi katika wilaya ya Bagamoyo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaji Abuubakar Kunenge akisisitiza jambo wakati Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kutoa na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi katika eneo la Mapinga wilayani Bagamoyo tarehe 10 Agosti 2022.

"Watu hawa wanafahamika na kamati imewaorosdhesha Mhe. Mkuu wa mkoa nakulabidhi taarifa hii ili ushighulike na wote ambao wamekuwa wakikiuka maadili na kuvunja sheria kiasi cha kusababisha migogoro ambayo imekuwa ikileta maimivu makubwa kwa wananchi,"alisema Dkt.Mabula.

Hata hivyo, alisema baadhi ya migogoro ya ardhi katika eneo la Mapinga na maeneo mengine ya wilaya ya Bagamoyo imekuwa ikisababishwa na ununuzi wa ardhi unaofanywa haraka bila kujiridhisha umiliki halali wa eneo husika.

"Wanunuzi wananunua maeneo bila ya kufanya uhakiki katika ofisi za halmashauri lakini pale wanapogundua wametapeliwa ndipo huanza kupeleleka malalamilo yao kwenye ofisi za serikali,"alisema Dkt.Mabula.

Ametoa rai kwa wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za halmashauri na kufanya upekuzi wa kujua miliki kuanzia ngazi ya halmashauri kwa yale maeneo yenye hati.

Aidha, Dkt Mabula alitahadharisha wananchi wanaovamia mashamba na kubainisha kuwa uamuzi wa serikali kushughulikia mashamba pori haina maana ya kuruhusu uvamizi na kusisitiza kuwa ni marufuku wananchi kuvamia maeneo hata kama ni shamba pori.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainab Issa akizungumza wakati Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kutoa na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa migogoro ya ardhi katika eneo la Mapinga wilayani Bagamoyo tarehe 10 Agosti 2022. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).

Pamoja na kamati iliyoundwa chini ya mwenyekiti wake Kamishna Msaidizi wa Polisi Peter Matagi kushughulikia migogoro ya ardhi ya eneo la Mapinga lakini iliwasikiliza wananchi wengine kutoka maeneo mbalimbali ndani ya Bagamoyo yakiwemo ya kata ya Makurunge, Kidomole, Sanzale, Kerege, Mataya, Ukuni na Fukayosi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakar Kunenge alimueleza Waziri wa Ardhi Kuwa mkoa wake utaanza kuifanyia kazi taarifa hiyo kwa kuwashughulikia wote waliohusika bila kujali nyadhifa ya mtu na kusisitiza kuwa hakuna mtu atakayeonewa wakati wa kushughulikia mgogoro huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news