Waziri Mkuu aungana na mamia ya Watanzania kuaga mwili wa Augustino Lyatonga Mrema

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kumkumbuka Mhe. Augustino Lyatonga Mrema kutokana na mchango wake mkubwa wa kuendeleza mahusiano na vyama vya siasa.

“Mheshimiwa Mrema atakumbukwa kama kiongozi mkuu wa Chama cha TLP kwa muda mrefu sana. Na akiwa katika siasa, aliisaidia Serikali kupata mwelekeo mzuri wa vyama vya siasa;

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho wakati kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) marehemu Augustine Lyatonga Mrema, kwenye Kanisa la Roman Catholic Salasala, jijini Dar es Salaam, Agosti 24 2022. (Picha na Ofisi ya Wziri Mkuu).

Ametoa kauli hiyo leo mchana Agosti 24, 2022 wakati akizungumza na mamia ya waombolezaji kwenye ibada ya kumuaga marehemu Mrema katika Parokia ya Mt. Augustino Kilimahewa, Salasala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Amesema salamu za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliwasilishwa asubuhi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

"Sisi tuliopo hapa tuna mambo mawili makubwa ya kufanya ili kumuenzi ndugu yetu Mrema. Moja ni kuenzi yale yote aliyofanya kwa upande wa Serikali na upande wa siasa lakini pili, tuendelee kumuombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho yake mahali pema peponi," amesema.

Kuhusu mazishi yake yanayotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi huko Kiraracha, Moshi, Waziri Mkuu amesema Serikali itawakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Hamad Masauni.

Akizungumza na niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mkuu wa Utawala wa Jeshi hilo, DCP Anthony Luta alisema Jeshi la Polisi litaendelea kumkumbuka Mhe. Mrema kwa mambo kadhaa ikiwemo hatua yake ya kuanzisha jeshi la ulinzi wa sungusungu, ujenzi wa vituo vidogo vya polisi na utetezi wa haki za wanawake ambapo kwa sasa wameanzisha madawati ya jinsia kwenye vituo vya polisi.

Naye Paroko wa kanisa hilo, Padre Peter Assenga alisema Mhe. Mrema alikuwa akijitolea kwa mambo mengi parokiani hapo na ataendelea kukumbukwa sana.

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alisema umati mkubwa uliokuwepo kanisani hapo ni ishara tosha ya jinsi Bw. Mrema alivyoishi vizuri na watu wakiwemo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu mmoja na mapadre sita. Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Hamad Rashid, Prof. Ibrahim Lipumba, John Cheyo, Steven Wassira, James Mbatia, Joseph Selasini na Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news