NA MWANDISHI WETU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, leo 25 Agosti 2022, ameelekea nchini Tunisia, kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD.
Mkutano huo utakaofanyika tarehe 27 na 28 Agosti, 2022 unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na ajenda za kimaendeleo zitakazotekelezwa kati ya Japan na Afrika.
Tanzania imekuwa ikishiriki mikutano hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993. Kufuatia mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Japan hususani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Tanzania imekuwa ikinufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, maji, elimu, afya na kilimo.
Kwa upande wa Afrika, mkutano huo unafanyika kwa mara ya pili baada ya ule wa mwaka 2016 uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.
Kupitia mkutano wa Saba uliofanyika Yokohama, Japan mwaka 2019, Japan ilitenga Dola za Marekani bilioni 20 kwa ajili ya kufanikisha malengo mbalimbali ya kimaendeleo kwa kipindi cha miaka mitatu (2019-2022).