NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene ameomba wananchi kuenzi mambo mema yaliyoachwa kama alama wakati wa uhai wa Augustino Lyatonga Mrema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akitoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa hayati Augustino Lyatonga Mrema.
“Tunamkumbuka kwa uzalendo wake wa kupenda demokrasia, lakini pia kupenda amani na utulivu katika itikadi zote. Mrema ni mtu mwenye rekodi kubwa katika siasa za ushindani wa nchi yetu”
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akitoa salamu za Serikali katika ibada ya maziko ya hayati Augustino Lyatonga Mrema iliyofanyika Marangu-Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akitoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa hayati Augustino Lyatonga Mrema.
"Sisi kama serikali tunaungana nanyi katika wakati huu mgumu; kushiriki msiba kwa moyo mkuu maana sisi sote tunakwenda safari hiyo, yeye ametangulia sisi tupo nyuma yake, alisema waziri,"amesema.
Ameeleza serikali na viongozi wakuu wanawapa pole Mama Watoto wa Marehemu na Wanakiraracha kwa ujumla na kipekee sana wanachama wote wa TLP, chama ambacho amefariki akiwa ni Mwenyekiti wake wa Kitaifa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene akitoa salamu za pole kwa niaba ya serikali katika ibada ya mazishi ya hayati Augustino Lyatonga Mrema iliyofanyika Marangu-Vunjo.
“ Marehemu Mrema amefariki akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole,na amefanya kazi yake vizuri alisema Waziri,”amesema.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Mhasham Baba Askofu Ludovick Minde, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Padri Deogratius Matiika wakili wa Askofu Jimbo Katoliki Moshi ametoa pole kwa wanafamilia na wale wote walioguswa na msiba.
Waziri Mkuu mstaafu, Mzee John Samweli Malecela akiweka shada la maua kwenye kaburi la Agustino Lyatonga Mrema.(Picha na OWM).
"Sisi kazi yetu kubwa ni kuendelea kumuombea ili Mwenyezi Mungu ampe furaha mbinguni, ameshiriki na sisi katika maendeleo ya jimbo letu, na tunashukuru Mungu kwa hayo aliyoyafanya.
“Nawaomba wanafamilia Mshikamane baba ameondoka msije mkagombana, mkae kwa amani na upendo,"amesema Padri Matiika.